Akizungumza na IQNA, Sheikh Zuhair al-Jaid, mratibu mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Al-Amal al-Islami nchini Lebanon amesema kuwa katika Sira ya Mtume Muhammad (SAW), mtu anaweza kuona kwamba yeyote anayesilimu anatendewa mema sana hata kama yeye ni kafiri moyoni.
Amebainisha kuwa Mtukufu Mtume (SAW) hata hakuwatendea vibaya wanafiki maadamu walitamka kalima La Ilaha Illa Allah na Muhammad Rasul Allah (Hakuna apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah).
Alipoulizwa kuhusu njia za kivitendo za kuimarisha umoja wa Kiislamu, Sheikh al-Jaid alisema kunapaswa kuwepo juhudi za kujenga madaraja ili kuondokana na tofauti na kukuza ushirikiano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema Fitna za sasa katika ulimwengu wa Kiislamu zimetengenezwa na maadui na ili kuziondoa na kukabiliana na changamoto zinazoukabili Umma wa Kiislamu hivi leo, kunahitajika umoja wa Waislamu.
Matukio ya hivi majuzi katika eneo hilo, hasa uvamizi dhidi ya Palestina na Lebanon yanafanya kuwa muhimu zaidi kuimarisha umoja wa Kiislamu, alisema.
Kwa hivyo, kuimarisha umoja wa Kiislamu ni muhimu sio tu ili kuendelea kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sira ya Mtume (SAW) bali pia kwa mtazamo wa kisiasa, Khatibu huyo aliongeza.
Vile vile amepongeza Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lililofanyika mjini Tehran wiki iliyopita na kusema wakati wa mkutano huo, shakhsia na wanazuoni wa madhehebu za Shia na Sunni walikaa pamoja bila hitilafu yoyote na kudhihirisha umoja wao.
"Tunaweza kuondoa Fitna kupitia umoja wa Kiislamu kwa kusisitiza mambo yetu ya pamoja," alisisitiza.
Mkutano wa 38 wa Umoja wa Kiislamu uliandaliwa na Jukwaa la Kimataifa la Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu katika mji mkuu wa Iran Tehran mnamo Septemba 19-21.
Zaidi ya viongozi 200 mashuhuri wa Kiislamu kutoka kote Iran na nchi za Kiislamu walihudhuria hafla hiyo ya siku tatu ili kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi punde katika ulimwengu wa Uislamu, huku suala la Palestina likisalia kuwa kitovu cha mijadala hiyo.
3490007