IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Hizbullah haitafuata njia aliyokusudia adui ya vita vya ndani Lebanon

22:27 - August 04, 2021
Habari ID: 3474157
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ametahadharisha kuhusu njama za maadui za kuitumbukiza nchi hiyo kwenye lindi la vita vya ndani vya wenyewe kwa wenyewe.

Sayyid Hassan Nasrallah ametoa indhari hiyo kufuatia matukio yaliyojiri hivi karibuni katika eneo la Khalda na akasema "kuna watu wanaotaka kuleta silaha kwa ajili ya kupambana na Hizbullah, lakini sisi hatutafuata kila njia aliyokusudia kutupitisha adui."

Itakumbukwa kuwa usiku wa kuamkia Jumapili ya wiki hii, watu wenye silaha waliufyatulia risasi umati wa watu waliokuwa wakishiriki kwenye mazishi ya mwanachama wa Hizbullah shahidi Ali Shibli katika eneo la Khalda kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, ambapo watu wanne waliuawa na wengine kumi walijeruhiwa.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameendelea kubainisha kuwa, kuisukuma harakati hiyo kwenye mapigano, kunamaanisha azma aliyonayo adui ya kuanzisha vita vya ndani nchini Lebanon na akaongeza kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, njama hiyo ya maadui ilianza tangu aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri alipowekwa kizuizini nchini Saudi Arabia.

Tarehe 4 Novemba 2017, Hariri aliwekwa kwenye aina fulani ya kizuizi nchini Saudia; na kwa mashinikizo ya utawala wa nchi hiyo akajiuzulu cheo chake cha uwaziri mkuu wa Lebanon.

3988481

captcha