Utafiti huo uliochapishwa Alhamisi na Shirika la Umoja wa Ulaya la Haki za Msingi (FRA) uligundua kuwa karibu nusu ya Waislamu barani Ulaya walikabiliwa na ubaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Ripoti ya FRA imeongeza kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa kasi, hasa katika mwaka uliopita huku taharuki zikiongezeka Asia Magharibi, ambapo sasa "ni vigumu zaidi kuwa Muislamu katika Umoja wa Ulaya."
Msemaji wa FRA Nicole Romain aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba: "Tunafahamu ripoti kutoka nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya, zinazoonyesha ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu," Hata hivyo, hata kabla ya kuongezeka, ripoti ya FRA ilibaini kuwa, "ilikuwa vigumu zaidi kuwa Muislamu katika Umoja wa Ulaya".
Naye mkurugenzi wa FRA Sirpa Rautio amesema: "Tunashuhudia ongezeko la kutisha la ubaguzi wa rangi na ubaguzi dhidi ya Waislamu barani Ulaya. " Ameongeza kuwa, "Hali hii inachochewa na mizozo ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na inafanywa kuwa mbaya zaidi na matamshi ya udhalilishaji dhidi ya Waislamu tunayoona katika bara zima. ."
Utafiti huo, ambao ulifanywa kabla ya utawala wa Israel kuanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza zaidi ya mwaka mmoja uliopita mapema Oktoba 2023, ulihusisha zaidi ya nchi kumi za Umoja wa Ulaya ambapo zaidi ya Waislamu 9,600 walihojiwa kati ya Oktoba 2021 na Oktoba 2022.
Katika uchunguzi huo, kiwango cha juu zaidi cha ubaguzi wa Waislamu kilikuwa nchini Austria, kikiwa ni asilimia 71.
Ujerumani, ambayo ni mwenyeji wa Waislamu wengi zaidi barani Ulaya, ilikuwa ya pili kwa asilimia 68, na Finland ya tatu kwa asilimia 63.
Ufaransa, ambayo inashika nafasi ya pili baada ya nchi jirani ya Ujerumani kwa idadi ya Waislamu wanaoishi nchini humo, ina kiwango cha kwa asilimia 39.
Ripoti ya FRA imeongeza kuwa watu barani Ulaya, wanawake na watoto , walilengwa sio tu kwa ajili ya imani yao ya kidini, bali pia rangi ya macho, nywele na ngozi zao, pamoja na sifa zingine za mwili.
"Wanawake wa Kiislamu, wanaume na watoto wanalengwa sio tu kwa sababu ya dini zao, lakini pia kwa sababu ya rangi ya ngozi zao na asili ya kabila au wahamiaji," FRA ilipendekeza katika ripoti yake.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Waislamu waliozaliwa katika Umoja wa Ulaya na wanawake wanaovaa mavazi ya kidini ya hijabu wanaathiriwa hasa na ubaguzi ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa kiholela wa polisi.
Waislamu milioni ishirini na sita wanaishi katika Umoja wa Ulaya unaojumuisha zaidi ya asilimia 5 ya wakazi milioni 448 wa nchi za umoja huo.
3490414