IQNA

Umoja wa Mataifa

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Uenezaji Chuki Dhidi ya Uislamu katika Umoja wa Mataifa

22:29 - March 13, 2023
Habari ID: 3476699
TEHRAN (IQNA)- Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa uenezaji hofu juu ya Uislamu na chuki za aina mbalimbali dhidi ya Uislamu na Waislamu duniani.

Akihutubia mkutano maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Uenezaji Chuki Dhidi ya Uislamu, Antonio Guterres alisema: Kuna idadi ya Waislamu karibu bilioni mbili duniani ambao wanakabiliwa na chuki na ubaguzi kwa sababu tu ya imani yao.

Guterres amebainisha kuwa, ubaguzi huo unajidhihirisha katika unyanyapaa ulioenea dhidi ya jamii za Waislamu na maonyesho ya vyombo vya habari yenye upendeleo wa kuaibisha na matamshi na sera zilizo dhidi ya Uislamu za baadhi ya viongozi wa kisiasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza kwamba, "ubaguzi unatudhoofisha sote, hivyo ni wajibu kwa sisi sote kusimama kidete kukabiliana na ubaguzi".

Ukosoaji mkali wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu chuki dhidi ya Uislamu unatolewa katika hali ambayo, mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu umechukua mkondo mpana zaidi katika mataifa ya Magharibi. Propaganda na chuki dhidi ya Uislamu zimekuwa zikifanyika kwa mbinu na mikakati mbalimbali kama vile kufanyia dhikaha matukufu ya Kiislamu ikiwemo hatua ya kuchora vibonzo vinavyomvunjia heshima Bwana Mtume (saww), kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu kama kuchoma moto Qur'ani tukufu, kuonyesha sura hasi ya Uislamu na Waislamu, vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu hususan wanawake, hujuma mtawalia dhidi ya vituo na asasi za Kiislamu na misikiti na wigo mpana wa ubaguzi dghidi ya Waislamu katika mataifa ya Magharibi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ni jambo ambalo limekuwa likishika kasi na kuchukua wigo mpana zaidi siku baada ya siku katika nchi za Magharibi. Wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na lililoratibiwa limekuwa likidhihirika katika kalibu na muundo tofauti ulio rasmi na usio rasmi.

Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio maalumu na kuitangaza Machi 15 kuwa Siku ya Kimataifa ya kukabiliana na uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu (Islamopohobia), ikiwa ni hatua ya mabadiliko katika mapambano ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu katika ngazi ya kimataifa.

Marafiki wanaounga mkono Hati ya Umoja wa Mataifa walitangaza katika taarifa waliyotoa juzi Ijumaa katika mkutano wa pamoja wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu, kwamba: "tunapinga na kulaani aina yoyote ile ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa kwa sababu za dini au itikadi, utamaduni, utaifa au kabila na hali ya kijamii, kisiasa au kiuchumi.

Kundi hilo limesisitiza kuwa, ikiwa ni mara ya kwanza kuadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na chiki dhidi ya Uislamu ambapo kuanzia sasa siku hii itakuwa ikiadhimiswa tarehe 15 Machi kila mwaka, linatangaza kupinga kuitwa Waislamu kwa majina mabaya, taasubi na hujuma dhidi ya dini ya Kiislamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, licha ya kampeni kubwa na propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika mataifa ya magharibi, lakini Uislamu ndio dini inayokuwa kwa kasi katika mataifa hayo.

4127999

captcha