IQNA

Muqawama

Kiongozi: Iran itoa jibu kali kwa hatua yoyote dhidi ya taifa la Iran

19:37 - November 02, 2024
Habari ID: 3479685
IQNA-Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo ameeleza sababu za msingi za mapambano ya taifa la Iran yanayoendelea kwa takriban miaka 70 dhidi ya dhulma na sera za kupenda kujitanua za Marekani, na kusisitiza kuwa: Katika njia hiyo ya ushindi, utawala wa Kizayuni na Marekani watapewa jibu kali kwa hatua yoyote dhidi ya taifa la Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuadhimisha kumbukumbu ya kutekwa pango la ujasusi la Marekani (ubalozi wa Marekani mjini Tehran) uliotwaliwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran tarehe 4 Novemba 1979, inayojulikana kama Siku ya Kitaifa ya Mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimataifa.

Akihutubia hadhara ya maelfu ya wanafunzi wa Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pendekezo la mmoja wa wanachuo kuhusu jinsi ya kukabiliana na ubeberu. Amesema: Watu wote wanapaswa kujua kwamba, katika mapambano haya, kila hatua muhimu za kijeshi, silaha na kisiasa zitachukuliwa kwa ajili ya maandalizi na utayarifu wa taifa la Iran, na maafisa wanashughulikia masuala hayo kwa sasa.

Amesema mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu ni suala la kudumu na endelevu katika maisha ya taifa na kuongeza kuwa: Harakati jumla ya taifa na viongozi katika kukabiliana na ubeberu wa kimataifa na chombo cha kihalifu kinachotawala mfumo wa sasa wa dunia ni hatua ya kimantiki inayooana na Sharia, maadili na kanuni  za kimataifa, na taifa na viongozi hawatazembea hata kidogo katika suala hili.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja taarifa ya idadi kubwa ya jumuiya za kisayansi za wanafunzi wa vyuo vikuu huko Marekani dhidi ya utamaduni na ustaarabu wa nchi za Magharibi na hatua za Marekani, na kuzitetea nchi na mataifa yanayodhulumiwa kuwa ni ishara nyingine ya mafanikio na maendeleo ya harakati inayopinga ubeberu. Amesema: Mapambano haya yataongezeka siku baada ya siku, na watu wa Iran, mataifa yanayodhulumiwa na kambi ya Muqawama itapiga hatua zaidi za maendeleo.

Ayatullah Khamenei amesema, jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na mauaji ya watu 50,000 ambao wengi wao ni wanawake na watoto, na maafa yanayotokea hivi sasa nchini Lebanon, ambayo yote yanatekelezwa kwa msaada wa kijeshi na wa kisiasa na ushiriki wa Marekani, vimeweka wazi uongo na fedheha ya madai ya kutetea haki za binadamu ya nchi hiyo. Amesema, leo dunia imetambua kwamba, wahalifu wanaodai kutetea haki za binadamu, wanaowaita watu wakubwa kama Sayyid Hassan Nasrullah, Ismail Haniyeh na Kamanda Qassim Soleimani kuwa ni magaidi, wao wenyewe ni genge la kigaidi na genge la uhalifu.

Imam Ali Khamenei ameutaja umaarufu na kupendwa taifa la Iran katika maoni ya umma wa walimwengu, licha ya propaganda chafu na kubwa za vyombo vya habari vya mfumo wa ubeberu, kuwa ni ishara ya ufanisi wa mafanikio na mapambano ya kimantiki ya Jamhuri ya Kiislamu. Amesema: Hali ya watu kushangilia katika mitaa ya miji ya nchi mbalimbali baada ya kutekelezwa operesheni ya kijeshi ya Ahadi ya Kweli dhidi ya utawala haramu wa Israel ina maana kwamba, harakati ya taifa la Iran inakubaliwa na mantiki ya kimataifa, na bila shaka, mantiki ya Kiislamu na Qur'ani.

3490523/

captcha