Kwa mujibu wa Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatatu alipokutana na Maulamaa, Maimamu wa Swala ya Ijumaa pamoja na wakurugenzi wa Madrassah za Ahul Sunna kutoka kote Iran kwa munasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu sambamba na siku za kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW).
Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei amesema kuna udharura wa kulinda utambulisho wenye thamani wa 'Umma wa Kiislamu' na kusisitiza kuhusu umoja wa Kiislamu. Huku akiashiria njama za wasiowatakia mema Waislamu ambao wanavuruga umoja huo amesema: "Kadhia ya Umma wa Kiislamu haipaswi kusahauliwa."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Suala la utambulisho wa Umma wa Kiislamu ni suala la kimsingi ambalo linavuka utaifa na mikapa ya kijiografia." Amesisitiza kuwa uhakika na utambulisho wa umma wa Kiislamu haubadiliki."
Ayatullah Khamenei ameashiria njama za mahasimu za kuwafanya Waislamu wapuuze au wasijali kuhusu utambulisho wao wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu wakati Mwislamu anapoghafilika kuhusu masaibu ya Waislamu wenzake huko Gaza na maeneo mengine duniani."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito kwa Maulamaa wa Ahul Sunna, kufungamana na utambulisho wa Kiislamu na umma wa Kiislamu ambapo ameashiria pia mipango na harakati zenye historia ndefu za wasiowatakia mema Waislamu ambao wamekuwa wakiibua migonganao ya kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu na hasa nchini Iran na kusema: "Wanatumia mbinu za kiakili, kifikra, kipropaganda na kiuchumi ili kuwatenganisha Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni nchini na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu." Ametaja moja ya mbinu zinazotumiwa kuwagonganisha Waislamu kuwa ni kuwafanya wafuasi wa pande mbili kuhasimiana na kubishana ili hitilafu ziendelee kuwepo.
Ayatullah Khamenei amesema njia ya kukabiliana na njama hizi za maadui ni umoja na kuongeza kuwa: "Kadhia ya umoja si mbinu bali ni msingi wa Qur'ani."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema umma wa Kiislamu hauwezi kufikia lengo la kupata nguvu na hishima isipokuwa kwa kuwa na umoja.
Aidha amesema leo moja ya mambo ambayo bila shaka ni wajibu ni kuwaunga mkono wanaodhulumiwa huko Gaza na kote Palestina na iwapo yeyote atakwepa jukumu hili bila shaka Mwenyezi Mungu atamuuliza kuhusu suala hilo.
Ikumbukwe kuwa siku kama ya leo miaka 1499 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mas'udi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.
Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu), muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.
Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.
3489920