IQNA

Katika Ujumbe wa Mwaka Mpya wa 1403 Hijria Shamsia

Kiongozi Muadhamu: Matukio ya Gaza yanalihuzunisha taifa la Iran

13:38 - March 20, 2024
Habari ID: 3478549
IQNA-Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe muhimu kwa mnasaba wa Nowruz ambayo ni siku ya kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa 1403 Hijria Shamsia na ameuita mwaka huo kuwa ni wa kuongezeka kwa uzalishaji wa kiuchumi kwa kushirikisha wananchi.

Katika sehemu moja ya ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia masuala muhimu kwa Iran katika mwaka ulioisha wa 1402 Hijria Shamsa ambao umemalizika mapema leo asubuhi na kulitaja suala la vita vya Gaza na mateso wanayopata wananchi wa Palestina kuwa ni miongoni masuala machungu sana ya kimataifa kwa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amegusia pia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni mwezi wa machipuo ya kiroho na kimaanawi ambao mwaka huu pia umekwenda sambamba na kuanza msimu wa machipuo na mwaka mpya wa Hijria Shamsia na kuhimiza kufanyika jitihada kubwa zaidi ya mwaka ulioisha wa 1402 Hijria Shamsia katika kuliletea maendeleo ya kila upande taifa. 

Kuhusu mwaka huu mpya ulionza saa chache zilizopita wa 1403 Hijria Shamsia, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, huu ni mwaka wa "Ustawi wa Uzalishaji kwa Kushirikisha Wananchi" na kusisitiza kuwa kila mmoja anapaswa aweke ahadi ya kutekeleza kikamilifu majukumu yake katika nyuga tofauti kwa ajili ya kutatua masuala ya wananchi hasa ya kiuchumi na amewaombea wote mwaka uliojaa baraka, amani na mafanikio.

Ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe wa Mwaka Mpya wa Kiongozi Muadhamu

 

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.

Ewe unayebadilisha nyoyo na macho ya watu. Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana! Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.

 

Napenda kutoa pongezi zangu kwa taifa zima la Iran kwa ujio wa Nowruz na mwanzo wa mwaka huu mpya ambao mwaka huu umesadifiana na mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni machipuo ya nyoyo na machipuo ya kiroho (kimaanawi). Ningependa hasa kutoa pongezi zangu kwa familia za maveterani wa vita pamoja na mataifa mengine yote yanayosherehekea Nowruz.

Pia ningependa kutoa heshima zangu kwa mashahidi wetu wapendwa na Imam (Khomeini MA) wa Mashahidi, ambao walifungua njia hii kwa ajili ya taifa la Iran. Natumai taifa la Iran litafaidika na machipuo yote mawili – machipuo ya mazingira  na machipuo ya kiroho.

Hebu tupitie mwaka wa 1402 Hijria Shamsia [Machi 2023 - Machi 2024], ambao umemalizika hivi punde, na tuangalie mwaka ambao tumeingia hivi punde. Mwaka wa 1402, kama miaka mingine yote ya maisha yetu, ulijawa na nyakati tamu na chungu. Ulijawa na matukio ya yanayofaa na yasiyofaa.

Hii ndiyo asili ya ulimwengu na asili ya maisha yenyewe. Katika masuala ya ndani ya nchi, tuliona maendeleo makubwa kote nchini katika nyanja za sayansi, teknolojia na miundombinu ya kimsingi. Haya yalikuwa baadhi ya mambo ya kupendeza ambayo tulipitia. Kwa upande mwingine, matatizo ambayo watu walikumbana nayo kuhusu uchumi na maisha yao ni baadhi ya matukio machungu ambayo tuliyashuhudia.

Ushiriki mkubwa wa Wairani katika hafla za kitaifa

Ushiriki mkubwa wa watu katika mjumuiko wa Siku ya Quds na maandamano ya 22 ya Bahman (11 Februari), ambayo ilikuwa mijumuiko hii ya ajabu iliyofanyika kwa usalama, uchaguzi nao ulifanyika kwa usalama na bila dosari uchaguzi mwishoni mwa mwaka, ambapo umma ulionyesha uwepo wao, yalikuwa baadhi ya matukio ya kupendeza, ya kutamanika ambayo yalifanyika katika mwaka uliopita.

Tukio la kusikitisha lililotokea Kerman katika ukumbusho wa [mauaji] ya Shahidi Soleimani, mafuriko yaliyokumba Baluchestan mwishoni mwa mwaka, na matukio ambayo vikosi vyetu vya usalama na wasimamizi wetu wa usalama wamekumbana nayo katika miezi michache iliyopita yalikuwa miongoni mwa matukio machungu ambayo tulishuhudia katika mwaka uliopita. Na la kusikitisha zaidi kuliko yote ni tukio la kusikitisha linaloendelea Gaza - tukio ambalo lina umuhimu mkubwa katika masuala yetu ya kimataifa. Hatujawahi kushuhudia chochote cha kusikitisha zaidi ya tukio hilo la mwaka huu.

'Vita vya Gaza ni tukio la kusikitisha zaidi katika uga wa kimataifa’

Kuhusu masuala ya kigeni, hatua za serikali (ya sasa ya Iran) katika nyanja za kimataifa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa ni baadhi ya matukio ya kupendeza. Kama nilivyokwisha sema, tukio la kutisha huko Gaza halikuwa moja tu ya matukio ya kusikitisha zaidi bali pia lilikuwa tukio la kuhuzunisha zaidi kwetu katika uwanja wa kimataifa.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu afidie matukio haya machungu na aendelee kulijalia taifa la Iran na mataifa ya Kiislamu matukio ya kupendeza na ambayo ni chimbuko la kheri na baraka kwa Umma wa Kiislamu na taifa la Iran.

"Uchumi ni suala kuu"

Kuhusu kauli mbiu niliyotangaza mwaka 1402 Hijria Shamsiya, ambayo ilikuwa "Udhibiti wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uzalishaji," hatua nzuri zimechukuliwa. Mafanikio yamefikiwa kuhusu sehemu zote mbili za kauli mbiu. Na maendeleo yamepatikana, lakini sio kwa kiwango ambacho kilitarajiwa. Mwenyezi Mungu akipenda, nitalizungumzia hili kwa undani zaidi katika hotuba yangu ya leo kwa taifa la Iran.

Hatua zilizochukuliwa zilikuwa nzuri, lakini lazima ziendelee. Kauli mbiu hii sio ambayo tunapaswa kutarajia itatoa matokeo yanayohitajika katika mwaka mmoja tu. Jitihada zinapaswa kuendelea. Kuna kazi kubwa sana inayotakiwa kufanywa katika mwaka ulio mbele yetu ambao ndio kwanza tumeingia, na ni lazima tutimize wajibu wetu kuhusiana na kazi zilizopo.

Maafisa wa nchi yetu, wakiwemo  wa serikali, bunge, mahakama, umma, na wengineo - sote tunahitaji kutimiza wajibu wetu wa kazi mbalimbali katika maeneo mbalimbali. Lakini suala kuu ambalo nchi inakabiliwa tena mwaka huu ni uchumi. Udhaifu mkubwa wa nchi ni katika uwanja wa uchumi. Lazima tuwe na harakati katika uwanja huu.

'Uzalishaji ni ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi'

Baada ya kuchunguza maoni ya wataalam kuhusu maudhui hii, nimefikia hitimisho hili kwamba ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi ni katika uzalishaji - uzalishaji wa ndani, uzalishaji wa kitaifa. Hii ndiyo sababu tumezingatia sana uzalishaji katika miaka michache iliyopita. Iwapo ukuaji wa uzalishaji na maendeleo katika uzalishaji wa ndani utafuatiliwa kwa njia ifaayo, masuala mengi muhimu ya kiuchumi ya nchi, kama vile mfumuko wa bei, ajira, na thamani ya sarafu yetu ya taifa, yatatatuliwa kwa njia inayofaa.

Kwa hiyo, uzalishaji ni suala muhimu na ndiyo maana ninaangazia tena jambo hili mwaka huu. Natarajia, Mwenyezi Mungu akipenda, kwamba tutashuhudia kuongezeka kwa uzalishaji. Pamoja na hayo, ninaamini kwa kweli kwamba hatua hii kubwa halitafanyika bila kuwepo na ushiriki wa wananchi.

Mwaka Mpya ni mwaka wa 'Kuongezeka kwa uzalishaji kwa kuwashirikisha wananchi'

Ikiwa tunapanga kuongeza uzalishaji wetu kwa haraka, tunahitaji kuwashirikisha watu kikamilifu katika uchumi. Lazima tufungue njia kwa wananchi kushiriki katika uzalishaji kwa namna inayoonekana na kuondoa vikwazo vinavyozuia ushiriki wao.

Kuna uwezo mkubwa katika sekta ya umma, ambayo nitaelezea baadaye, Mwenyezi Mungu akipenda. Ni lazima uwezo huu uwe amilifu na utumike manufaa ya nchi na wananchi. Ni kwa sababu hii  kauli mbiu ambayo nimechagua kwa mwaka huu ni, "Ustawi wa Uzalishaji kwa Kuwashirikisha Wananchi." Hii ndiyo kauli mbiu ya mwaka huu. Natumai, Mwenyezi Mungu akipenda, kauli mbiu hii itatekelezwa kwa njia bora zaidi. Ni lazima kwa wale wanaopanga mipango ya nchi kuunda mipango, kwa wataalam kushirikiana kwa kutoa mawazo yao, na kwa wale wanaofanya kazi katika sekta ya uchumi, Mwenyezi Mungu akipenda, washiriki kikamilifu katika jitihada hii.

Ninaomba kwamba Mwenyezi Mungu alijaalie mafanikio makubwa kwa taifa pendwa la Iran, na kwa unyenyekevu natoa salamu zangu kwa Baqiyatullah, yaani Salio la Mwenyezi Mungu duniani  (na roho zetu ziwe mhanga kwa ajili yake). Ninamwomba Mungu aharakishe kudhihiri kwake tena kwani hii, italeta ahueni kwa wanadamu wote.

Salamu, rehema, na baraka za Mungu ziwe juu yenu.

3487668

captcha