IQNA

Maisha ya Nabii Isa (AS) katika Qur’ani/2

Unabii wa Isa (AS)

21:30 - December 28, 2024
Habari ID: 3479964
IQNA - Isa au Yesu (AS) aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwaita Wana wa Israili (Bani Israil) kuelekea katika Taudi au kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na pia kuwathibitishia kwamba alikuwa nabii kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika sehemu iliyopita, kuzaliwa kwa Isa (AS) kulijadiliwa na katika sehemu hii, utabiri wake na uwepo wake kati ya Wana wa Israeli utajadiliwa kutoka kwa mtazamo wa Qur’ani. Katika imani ya Kiislamu, nasaba ya Maryamu inarudi hadi kwa Nabii Suleiman (AS) na kupitia yeye kwa Nabii Yakub (AS). Kwa hiyo, katika Qur’ani Tukufu, Isa pia anachukuliwa kuwa mmoja wa manabii wa Bani Israil. Isa (AS) alipewa kazi na Mwenyezi Mungu kuwaita Bani Israel waweze kufuata itikadi ya Tauhidi ya kumpwekesha Mwenyezy au kuabudu Mungu mmoj na pia kuwathibitishia kwamba alikuwa nabii aliyetumwa na Mungu. Alifanya miujiza mbele yao. Miongoni mwa miujiza iliyotajwa katika Qur’ani Tukufu ni kufufua wafu, kupulizia udongo na kuugeuza kuwa ndege hai, kuponya vipofu wa tangu kuzaliwa na wenye ukoma, pamoja na kuwa na maarifa ya mambo yasiyoonekana. Miujiza hii inahusishwa moja kwa moja na Isa ambapo Mwenyezi Mungu katika Aya ya 49 ya Surah Al Imran: “Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini.”

Isa (AS) aliwaita watu kwenye Sharia mpya (imani), ambayo ilithibitisha mafundisho ya Nabii Musa (AS). Alibatilisha baadhi ya amri za Musa katika Torati kwa ajili ya kuwaadhibu na kuwa wakali kwa Wayahudi, na alitangaza ujio wa Nabii Muhammad (SAW). Mara nyingi aliwaambia Wana wa Israili: “Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!’” (Aya ya 6 ya Surah As-Saff)

Isa (AS) aliendelea kuwaita Wana wa Israil kuelekea kwenye Tauhidi na Sharia mpya mpaka alipochoshwa na kukataa kwao kuamini. Aliposhuhudia uasi na ukaidi wa watu, pamoja na kiburi cha makuhani na wanazuoni wa Kiyahudi kukataa wito wake, alichagua wachache waliokuwa na imani naye kuwa wafuasi wake, ili waweze kumsaidia katika misheni yake kwa ajili ya Mungu. “Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.” (Aya ya 14 ya Surah As-Saff)

3491217

Habari zinazohusiana
captcha