IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Qur'ani Tukufu yavunjiwa heshima nje ya Msikiti nchini Ujerumani

15:09 - July 12, 2023
Habari ID: 3477267
Huku Waislamu katika kona zote za dunia wakiendelea kulaani na kupinga tukio la hivi karibuni la kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu nchini Uswidi, Kitabu hicho kitukufu cha Waislamu kimechomwa moto na kutupwa nje ya Msikiti mmoja nchini Ujerumani.

Chama cha Waislamu wa Kituruki na Masuala ya Kidini nchini Ujerumani (DITIB) kimesema tukio hilo ovu la kuchukiza lilifanyika nje ya Msikiti wa Mimar Sinan katika mji wa Maulbronn, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Ulaya.

Osman Adibelli, Mkurugenzi wa Kamati ya Msikiti wa Mimar Sinan amesema kuwa, watu wenye misimamo ya chuki na kufurutu ada wakiwa ndani ya gari lililokuwa kwenye mwendo, walichoma moto nakala ya Qurani Tukufu na kuirusha nje ya msikiti huo katika jimbo la Baden-Wurttemberg.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na Adibelli imeeleza kuwa, tukio hilo la kuvunjiwa heshima Kitabu kitakatifu cha Waislamu lilifanyika asubuhi ya Julai 8 mwendo wa saa 10:45, kabla ya Swala ya Alfajiri.

Haya yanajiri wakati huu ambapo vitendo vya hujuma na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vinaripotiwa kukithiri mno si tu nchini Ujerumani na Uswidei, bali katika aghalabu ya nchi za Magharibi.

Hii ni katika hali ambayo, Ujerumani yenye jamii ya watu milioni 84, ndilo taifa la pili lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu Ulaya Magharibi baada ya Ufaransa.

Tume huru ya Ujerumani ilisema katika ripoti iliyotolewa karibuni kwamba, mateso yanayowapata Waislamu kutokana na kuongezeka ubaguzi katika jamii ya Ujerumani yanahalalisha kuchukua hatua madhubuti za kupambana na chuki na ubaguzi unaofanywa dhidi yao.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser, aliisema baada ya kupokea ripoti hiyo kwamba "wengi kati ya Waislamu milioni 5.5 nchini Ujerumani wanasumbuliwa na kutengwa na kubaguliwa katika maisha yao ya kila siku, ikiwa ni pamoja na chuki na kufanyiwa ukatili."

4154188

captcha