IQNA

Hamas yasisitiza kupinga kikamilifu mpango wa Trump kuhusu Gaza

16:23 - February 13, 2025
Habari ID: 3480213
IQNA-Harakati ya Mpambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekariri upinzani wake dhidi ya matamshi yaliyotolewa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu suala la kuwahamusha makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza kwa kisingizio cha kulijenga upya eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imeyataja matamshi hayo ya Trump kuwa ni ya kibaguzi na wito wa kufuta kaumu kwa shabaha ya kuangamiza mapambano ya ukombozi wa Palestina na kuwanyima watu wa Palestina haki zao za kitaifa.

Hamas imesema, mpango wa kuwafukuza watu wa Palestina kutoka Gaza hautafanikiwa, na kwamba utakabiliwa na msimamo mmoja wa Wapalestina, Waarabu na Waislamu ambao unapinga mipango yote ya kuwahamisha watu kwa mabavu.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekariri bila ya aibu pendekezo lake tata la kulinyakua na kulidhibiti eneo la Ukanda wa Ghaza, akisema amejitolea "kulinunua na kulimiliki" eneo hilo lililoharibiwa na vita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege ya Air Force One siku ya Jumapili, Trump alisema Gaza inapasa izingatiwe kama "eneo kubwa la mali isiyohamishika" na kusisitiza kuwa: Tumejitolea kuimiliki, kuichukua, na kuhakikisha kuwa Hamas hairudi tena. Hakuna kitu cha kukirudia tena. Ni eneo lililobomolewa."

Mnamo Februari 4, Trump alifichua katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya White House nia ya nchi yake ya kuutwaa Ukanda wa Gaza baada ya kuwahamisha wakazi wake wote wa Palestina na kuwapeleka katika nchi nyingine. Mpango huo umepingwa kikanda na kimataifa.

3491843

Kishikizo: donald trump hamas gaza
captcha