Basem Naim, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, ameongeza katika taarifa yake kwamba: "Gaza ni sehemu isiyoweza kutenganishwa ya ardhi ya Palestina na si mali inayoweza kupigwa mnada kwenye soko huru."
Amesisitiza kuwa, kuruhusiwa kuingia misaada ya kibinadamu huko Gaza ndilo sharti la chini kabisa la mazungumzo na utawala wa Kizayuni ambao umeweka mzingiro mkali katika Ukanda wa Gaza tangu mwanzoni mwa mwezi Machi.
Mjumbe huyo wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema kwamba sharti la chini kabisa la kufanya mazungumzo mazuri na ya maana ni kulitaka baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu lifungue vivuko na kuruhusu misaada ya kibinadamu, chakula na dawa kuingia Gaza.
Akizungumza kwenye mkutano wa kilele wa biashara nchini Qatar siku ya Alkhamisi, rais wa Marekani, Donald Trump alitoa matamshi ya kijuba akidai kuwa ataidhibiti Gaza na eti ataugeuza ukanda huo kuwa eneo huru.
Lakini Wapalestina wanakataa vikali mpango wowote ambao utapelekea wananchi wa Gaza kuondolewa kwenye eneo hilo, au kugeuzwa ukanda huo kuwa milki ya madola mengine. Wapalestina wanalinganisha njama hizo na jinai za "Nakba" yaani janga na nakama ya mwaka 1948, wakati mamia ya maelfu ya Wapalestina walipohamishwa kwa nguvu kwenye makazi yao ya jadi katika mashambulizi ya kijinai yaliyopelekea kuundwa dola pandikizi la Israel katika kitovu cha Ulimwengu wa Kiislamu.
4282721