Akizungumza na vyombo vya habari, Reza Khorakian, meneja mwandamizi wa haram hiyo, amesema kuwa "kila siku wakati wa Wiki ya Karamat, wafanyakazi wapatao 4,800 na wasaidizi wa kujitolea watatoa huduma katika maeneo 62 tofauti kwa ajili ya kusaidia wafanyaziara."
Wiki ya Karamat huadhimisha kumbukumbu za kuzaliwa kwa Hadhrat Masoumah (SA) na Imam Ridha (AS), ambazo mwaka huu zinaangukia Aprili 29 na Mei 9, mtawalia. Ni kipindi cha ziyara, sherehe na matukio ya kitamaduni, hasa katika miji ya Mashhad na Qom iliko Haram ya Hadhrat Masoumah (SA).
Miongoni mwa shughuli zilizopangwa, Khorakian amesema, ni sherehe za kila siku za kuzaliwa zinazoanza Jumanne. "Katika hafla ya kuzaliwa kwa Hadhrat Masoumah (SA), tutakuwa na sherehe za kuwakaribisha wasichana wachanga katika haram takatifu, pamoja na tukio maalum la kuwaheshimu wanawake vijana bora," alieleza.
Maandalizi ya wiki hiyo yalianza mapema kwa sherehe ya kufagia na kupuliza manukato katika kaburi la Imam Ridha (AS). "Haram imeandaliwa tayari kuwapokea wageni wakati wa sherehe hizo," alisema Khorakian.
Moja ya mambo muhimu yatakuwa kubadilisha bendera ya haram hiyo. "Tukio hili litafanyika Ijumaa, Mei 9, saa Moja asubuhi katika Uwanja wa Enghelab na litarushwa moja kwa moja kupitia vituo vya runinga vya ndani na vya kimataifa, pamoja na majukwaa makubwa ya mtandaoni," Khorakian alibainisha.
Programu maalum za Qur’ani zinazolenga wanawake na vijana pia zitafanyika, zikijumuisha ushiriki wa wasomaji maarufu na vipaji vya vijana.
Kwa upande wa kitamaduni, kitabu kipya kinachoitwa ‘The Sun Up Close’ kitazinduliwa. "Kitabu hiki kina maelezo ya safari 21 yaliyochaguliwa kutoka visa vya kweli vya wasafiri 200 wasio Waislamu waliotembelea mji mtakatifu wa Mashhad kwa karne nyingi," amesema Khorakian.
Katika kipindi cha wiki hiyo, vitabu na bidhaa za kitamaduni zipatazo 550,000, hasa zilizotengenezwa kwa ajili ya watoto na vijana, zitasambazwa.
Jitihada za kuwashirikisha wageni wa kimataifa pia zimeongezwa. "Programu za kila siku kwa lugha za Kiarabu, Kiurdu na Kiazeri zitafanywa kwa ajili ya wafanyaziara wasio Wairani," Khorakian amebaini.
3492868