Imam Ridha (AS) alitegemea mbinu mbalimbali wakati wa kutumia aya za Qur'ani katika hoja zake. Wakati mwingine, alikuwa akifafanua maana za wazi na zilizofichika za aya hizo kupitia tafsiri sahihi, akijibu waliokuwa na shaka kuhusu Qur’ani Tukufu. Katika matukio mengine, angethibitisha ukweli wa bishara za Qur'ani kwa kuzihusisha aya hizo na matukio ya kihistoria.
Kwa kutegemea aya zisizo na shaka (Muhkamat) za Qur’ani, Imam Reza (AS) alizifafanua aya zenye utata (Mutashabihat) na kushughulikia baadhi ya mashaka yaliyoibuliwa dhidi ya Uislamu.
Zaidi ya hayo, katika mazungumzo yake na wafuasi wa dini nyingine za kimungu, angerejelea mistari iliyopo katika maandiko yao pia. Kwa mfano, angerejelea umoja wa asili na madhumuni ya dini, akitaja vitabu vitakatifu vya imani nyingine.
Imam Ridha (AS), kwa kutumia aya za Qur'ani, alitoa dalili za Tauhidi au upweke na umoja wa Mwenyezi Mungu, akakataa ushirikina na kuabudu masanamu, akazungumzia maisha ya baada ya kifo na ufufuo, akathibitisha utume wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, hususan Mtume Muhammad (SAW), miujiza, pamoja na Uimamu na Ahlul-Bayt (AS). Pia alieleza sheria na kanuni za Kiislamu, akishughulikia mashaka yoyote katika maeneo haya.
Kwa mfano, pingamizi moja lililotolewa wakati wa mjadala na mwanachuoni wa Kikristo lilikuwa kwamba Mtume Muhammad (SAW) hawezi kuwa nabii kwa sababu kitabu kitakatifu alichoteremshiwa hakikuwa katika Kiebrania. Imam Ridha (AS) akinukuu aya: “Hatukumtuma Mtume yeyote ila kwa lugha ya kaumu yake ili awabainishie” (Sura Ibrahim aya ya 4), amesisitiza kuwa Mwenyezi Mungu hutuma Mitume kwa lugha ya watu wao ili ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwanza uweze kueleweka vyema kwao kabla ya kuenea maeneo mengine. Kwa vile Waarabu walikuwa walwengwa wa kwanza wa Mtume Muhamamd (SAW), Qur’ani Tukufu iliteremshwa kwa Kiarabu.
Kitabu hiki ni muujiza mkubwa, na hata kama hakikuwa katika Kiarabu, bado kingewea kuwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu maaadamu aliyeteremsihwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
3489755