IQNA

Iran yasitisha safari za ndege za kurejea kwa Mahujaji baada ya mashambulizi ya Israel

19:15 - June 13, 2025
Habari ID: 3480829
IQNA-Shirika la Hajj na Hija la Iran limetangaza Ijumaa kwamba safari zote za kurudi kwa Mahujaji wa Kiirani zimesitishwa hadi taarifa nyingine itakapotolewa, kufuatia kusimamishwa kwa safari za anga kote nchini baada ya mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Israel.

Kwa mujibu wa shirika hilo, hali ya dharura iliyosababishwa na kufungwa kwa anga ya Iran imezuia mipango ya kuwarejesha Mahujaji walioko Saudi Arabia. Kwa hivyo, mipango inafanywa ili kuongeza muda wa ukaaji wa Mahujaji wa Kiirani katika hoteli zao huko Makka na Madina.

"Operesheni za kurudi kwa Mahujaji hazitaendelea leo kutokana na kusimamishwa kwa safari za ndege," shirika hilo lilisema katika taarifa. "Taarifa muhimu kuhusu kuanza tena kwa safari za ndege zitatolewa baada ya matangazo kutoka kwa mamlaka husika."

Tangazo hili linakuja baada ya utawala wa Israel kufanya mashambulizi alfajiri ya leo katika maeneo kadhaa ya Iran, ikiwemo mji mkuu, Tehran. Milipuko imeripotiwa katika miji mbalimbali, huku video na picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha uharibifu mkubwa na huduma za dharura zikijibu matukio hayo. Idadi rasmi ya waathirika bado haijatolewa, lakini kuna wasiwasi mkubwa juu ya madhara kwa raia.

Miongoni mwa waliouawa shahidi katika mashambulizi hayo ni maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Iran, akiwemo Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Iran, na Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Ripoti pia zinaonyesha kuwa vituo vya kijeshi na vya nyuklia, ikiwemo kituo cha nyuklia cha Natanz, vililengwa katika mashambulizi hayo.

Kufuatia mashambulizi hayo, Iran ilifunga anga yake, ikisitisha safari zote za ndege za ndani na kimataifa.

Zaidi ya Waislamu milioni 1.6 kutoka kote duniani, wakiwemo takribani 86,000 kutoka Iran, walishiriki katika Hija ya mwaka huu, ambayo ilihitimishwa siku chache zilizopita.

4288176

Kishikizo: hija iran
captcha