IQNA

Pazia la Kaaba limebadilishwa kwa mnasaba wa kuanza mwaka wa Kiislamu 1447 Hijria

23:41 - June 25, 2025
Habari ID: 3480857
IQNA – Pazia la Kaaba Tukufu ambalo linajulikana kama Kiswa, linabadilishwa wiki hii kuashiria kuanza kwa mwaka wa Kiislamu wa 1447 AH.

 

Urais  wa Masuala ya Msikiti Mkuu wa Makka  na Msikiti wa Mtume (SAW) umetangaza kwamba mchakato wa kubadilisha Kiswa unafanyika Alfajiri siku ya Alhamisi, siku ya kwanza ya Muharram katika kalenda ya Hijria Qamaria.

Kiswa ya zamani imetolewa baada ya swala ya Alasiri siku ya Jumatano, tarehe 29 Dhu Al-Hijjah.

Kiswa, kitambaa kikubwa cheusi cha hariri kilichonakshiwa na aya za Qurani, hubadilishwa mara moja kwa mwaka katika utamaduni ulioanza karne nyingi zilizopita.

Kiswa hutengenezwa kila mwaka katika Kiwanda Maalum cha Mfalme Abdulaziz cha kutengeneza Kiswa ya Kaaba, kikitumia hariri asilia yenye rangi nyeusi ya hali ya juu. Kiswa huwa na urefu wa mita 14 na ukanda (hizam) mpana wa sentimita 95 ulioandikwa aya za Qur’ani kwa uzi wa dhahabu.

Ukanda huo hupita katika theluthi ya juu ya Kiswa na umeundwa kwa vipande 16 vinavyofikia urefu wa jumla wa mita 47.

Sherehe hii na ubadilishaji wa Kiswa ni sehemu ya urithi wa kiroho na kitamaduni wa Kiislamu unaozingatiwa kwa heshima kubwa kila mwaka mjini Makkah.

Kishikizo: kiswa
captcha