IQNA

Ndege za kuwarejesha Mahujaji wa Kiirani zaanza tena safari

21:16 - June 28, 2025
Habari ID: 3480862
IQNA – Operesheni ya kuwarejesha Mahujaji wa Kiirani wa Hija nchini kwa njia ya anga ilianza tena Alhamisi.

Ijumaa ilikuwa miongoni mwa siku zenye shughuli nyingi zaidi katika mchakato wa kuwarejesha Mahujaji nchini kwa ndege, ambapo kulikuwa na safari 10 za moja kwa moja kutoka Madina hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mashhad, kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Barabara na Maendeleo ya Mijini ya Iran. Safari za ndege katika anga ya Iran zilikuwa zimesitishwa kwa wiki mbili kutokana na hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Majid Akhavan alisema kuwa safari za ndege kutoka Madina hadi Mashhad siku ya Ijumaa zilisafirisha takribani Mahujaji 2,500 kurudi Iran.

Alibainisha kuwa operesheni ya kuwarejesha Mahujaji kwa ndege, ambayo ilikuwa imesimama kwa muda wa siku kumi na mbili kutokana na vita vilivyoanzishwa na utawala wa Israel, ilianza tena Alhamisi, Juni 26, na inatarajiwa kukamilika Julai 1.

Amesema mahujaji watarudi kwa kutumia ndege za moja kwa moja za Iran Air kutoka Uwanja wa Ndege wa Madina hadi Mashhad, na kisha kusafirishwa kwa barabara hadi mikoa yao ya nyumbani.

Msemaji huyo pia alieleza kuwa tangu kuanza kwa vita hivyo, mahujaji wamekuwa wakirudi kwa njia ya barabara kupitia Iraq, kutokana na juhudi za mara kwa mara za Shirika la Matengenezo ya Barabara na Usafirishaji, na mchakato huo umeendeshwa kwa ustadi, kwa mpangilio mzuri na bila matatizo yoyote.

Awali, Shirika la Hija na Mahujaji la Iran lilisema kupitia taarifa, "Kufuatia kughairiwa kwa safari za ndege na kushindwa kutumia usafiri wa anga, shirika lilichunguza njia zote salama za kuwarejesha mahujaji na hatimaye likapitisha mpango wa usafiri wa mchanganyiko wa anga na barabara ili kurahisisha kurejea kwao."

Kulingana na mpango huo—ulioandaliwa kwa ushirikiano na serikali ya Saudi Arabia—Mahujaji wanasafirishwa kwa ndege umbali wa kilomita 1,000 kutoka Madina hadi Uwanja wa Ndege wa Arar ulioko karibu na mpaka wa Iraq kwa kutumia ndege za Saudi. Kisha husafirishwa kwa mabasi yaliyopangwa hadi Najaf au Karbala, taarifa iliongeza.

Baada ya mapumziko mafupi na kutembelea maeneo matakatifu katika miji hiyo, mahujaji husafirishwa kwa mabasi hadi mipaka ya Iran, na baadaye hadi mikoa yao.

Shirika la Hija na Mahujaji limesema litatoa huduma zote muhimu wakati wa safari ya mpito nchini Iraq, ikiwa ni pamoja na chakula, huduma za afya, na hata intaneti ya simu kwa mahujaji.

Mwaka huu, takribani Wairani 86,700 walishiriki katika ibada ya Hija iliyofanyika huko Makka mapema mwezi Juni.

3493610

Kishikizo: iran mahujaji
captcha