Mohammed Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amesema hayo leo Jumapili mwanzoni mwa kikao cha Bunge na kusisitiza kwamba, "Leo hii, Gaza ni mji mkuu wa nyoyo za Waislamu wote duniani na kigezo cha kutofautisha Uislamu wa kweli na Uislamu wa maigizo na unafiki."
Aidha amesema hitaji la kimsingi la Masunni, Mashia na wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu ni kukomesha mauaji ya halaiki ya muda mrefu zaidi katika historia ya binadamu, ambayo ni mauaji ya kimbari ya miaka 80 ya watu wa Palestina yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na wahalifu waliobobeba na makatili wa Kizayuni.
Spika wa Bunge la Iran ameleeza bayana kuwa, "Utawala wa Kizayuni ambao ni fedheha kwa ubinadamu, haufahamu kitu kingine chochote isipokuwa lugha ya mabavu." Qalibaf amesema kuwa, uungaji mkono wa serikali za Magharibi kwa Israel, hasa Marekani, unahimiza utawala huo kuendelea na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Kadhia ya Palestina inatazamiwa kuwa mada kuu kwenye Kongamano la 38 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu litakaloanza Alkhamisi katika mji mkuu wa Iran, wakati wa Wiki ya Kimataifa ya Umoja wa Kiislamu.
Siku ya 17 ya Rabiul Awwal, ambayo ni Septemba 21 mwaka huu, inaaminika na Waislamu wa madhehebu ya Shia kuwa siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Mohammad (SAW), wakati Waislamu wa Sunni wanaamini tarehe sahihi ni 12 Rabiul Awwal. Muda kati ya tarehe hizo mbili huadhimishwa kila mwaka kama Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
Hayati Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (RA) ndiye alitangaza muda baina ya tarehe hizo mbili kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu nyuma katika miaka ya 1980.
3489901