IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Hujjatul Islam Shahriari atoa wito wa kuanzishwa Umoja wa Nchi za Kiislamu

11:57 - December 13, 2024
Habari ID: 3479894
IQNA-Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuunda umoja na kujitahidi kuungana ili kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Akihutubia mkutano wa kimataifa nchini Malaysia, Hujjatul Islam Hamid Shahriari alisema kwa umoja, mataifa ya Kiislamu yanaweza kutekeleza wajibu wao katika mpangilio mpya wa dunia na kutambulisha maadili ya Kiislamu duniani.

Mkutano wa ‘Kundi la Maono ya Kimkakati: Ulimwengu wa Kiislamu na Russia' ulifanyika mjini Kuala Lumpur siku ya Jumatano na Alhamisi kwa kushirikisha wawakilishi kutoka nchi 32 na mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa.

Hujjatul Islam Shahriari pia alisema kuibuka kwa utaratibu au mfumo mpya wa dunia kumetoa changamoto kwa utawala wa kibeberu wa Marekani wenye kuchukua maamuzi ya upande mmoja na kupelekea kuibuka kwa madola mapya yenye nguvu kieneo na kimataifa ambayo yanaahidi mabadiliko makubwa.

Akizungumzia uhalifu wa Marekani na upendeleo wa upande mmoja ambao umesababisha vifo vya mamilioni ya watu wasio na hatia duniani, amesema mbinu zilizopitishwa kwa ajili ya kufikia amani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia zimethibitisha kuwa hazifanyi kazi. Amesema kuna haja ya kuwepo mfumo mpya wa dunia ambao msingi wake ni haki na uadilifu.

Kwa msingi huo amependekeza  kuanzishwa kwa baraza la haki badala ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la sasa.

Aidha amesema alisema nchi za BRICS zinaweza kuja na mbinu sahihi za kuunda baraza hilo.

Aidha  amesema kuungwa mkono utawala wa Israel na wakuu wa baadhi ya mataifa kuwa ni kikwazo kikubwa cha kupatikana amani ya haki na endelevu duniani.

4253789

captcha