IQNA

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaendelea

14:44 - October 30, 2020
Habari ID: 3473310
TEHRAN (IQNA) - Mkutano wa 34 wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza kufanyika mjini Tehran ukihudhuriwa na shakhsia 167 wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kongamano hilo lililoanza jana Alhamisi linatarajiwa kuendelea hadi Jumanne ijayo yaani tarehe tatu Novemba ambapo aghalabu ya vikao hivyo vinafanyika kwa njia ya intaneti ili kuzuia maambukizi ya corona.

Shakhsia 167 wa ulimwengu wa Kiislamu kutoka nchi 47 pamoja na washiriki wengine 120 wa ndani wanatarajiwa kuhutubia katika mkutano huo ambao mara hii nara na kaulimbiu yake ni 'Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Maafa na Majanga'.

Kati ya waliohutubu katika sherehe za ufunguzi kwa njia ya intaneti nia Ayatullah Makarem Shirazi, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran Dkt. Mohammad Baqeri Qalibaf na Hujjatul Islam wal Muslimin Dkt. Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.

Miongoni mwa ajenda kuu zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa mara hii ni ushirikiano wa Kiislamu katika kukabiliana na majanga na masaibu, usaliti wa Wamagharibi kwa matukufu ya Palestina, nafasi ya mhimili wa muqawama katika kusambaratisha taathira za kuanzisha baadhi ya mataifa ya Kiarabu uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kadhalika mchango wa kamanda mkubwa wa Uislamu Luteni Jenerali Qassim Suleimani katika kuleta umoja na usalama wa ulimwengu wa Kiislamu.

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW.

3931881

captcha