IQNA

Qari Mwandamizi: Mashindano ya Qur'an Kama ‘Zayin al-Aswat’ huwapa vijana hmasa

20:24 - October 07, 2025
Habari ID: 3481337
IQNA – Mashindano ya Qur'an kama ‘Zayin al-Aswat’ huwapa vijana msukumo wa kiroho na hutoa kipimo sahihi cha maendeleo yao katika usomaji wa Qur'an, amesema Qari maarufu kutoka Iran, Ahmad Abolqassemi.

Katika mahojiano, Abolqassemi alieleza kuwa washiriki wa mashindano haya hupata maandalizi na tajriba muhimu ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'an. Toleo la kwanza la mashindano ya Zayen al-Aswat lilifanyika katika mji mtukufu wa Qom mnamo Oktoba 1–2, 2025.

Zaidi ya waombaji 1,600 kutoka mikoa yote 31 walijiandikisha, huku 94 wakifika hatua ya fainali. Washiriki wenye umri kati ya miaka 14 hadi 24 walishindana katika aina mbalimbali za usomaji wa Qur'an chini ya usimamizi wa majaji wa kimataifa.

Mashindano hayo, yaliyoandaliwa kwa kauli mbiu “Qur'an, Kitabu cha Waumini,” yaliratibiwa na Kituo cha Masuala ya Qur'an cha Taasisi ya Al al-Bayt kwa usaidizi wa taasisi za kitamaduni na za Qur'an. Usomaji wote ulirekodiwa na utachapishwa kupitia majukwaa ya vyombo vya habari vya taasisi hiyo.

Abolqassemi alitaja mashindano haya kuwa mwanzo muhimu wa kuleta mapinduzi katika uwanja wa mashindano ya Qur'an, na kuyachukulia kama hatua ya kuendeleza utamaduni safi wa Qur'an. “Ili jamii ipige hatua, inahitaji mfano wa kuigwa na mashujaa wanaojengwa katika mazingira ya mashindano yenye afya. Mashindano kama Zayen al-Aswat hutoa fursa ya kipekee ya kutambua na kuwasilisha vipaji angavu kwa jamii.”

Aliongeza kuwa “katika nchi yetu, wasomaji wa Qur'an hawatumiki ipasavyo kulingana na uwezo wao. Hali hii hupunguza motisha kwa wale walioko katika njia hii ngumu. Msomaji wa Qur'an huhitaji majukwaa mbalimbali kuonyesha uwezo wake ili kudumisha hamasa na juhudi endelevu.”

Abolqassemi alieleza kwa masikitiko kuwa “katika hafla nyingi za umma na binafsi, uwezo wa kipekee wa usomaji wa Qur'an kuleta mazingira ya kiroho na ya kukumbukwa hautumiki. Uzoefu wa moja kwa moja umeonyesha kuwa kila mkusanyiko ambapo usomaji wa Qur'an umepewa nafasi yake halali, hadhira imeupokea kwa shauku kubwa.”

“Ni jambo la kawaida kwamba pale ambapo nafasi hii haijatolewa kwa qari, motisha na matumaini hupungua.”

Aliona mashindano ya Zayen al-Aswat kama suluhisho muhimu la kuziba pengo hili, akisema: “Mashindano haya huwapa vijana msukumo na maana ya maisha, na hutoa kipimo sahihi cha maendeleo yao binafsi. Zaidi ya hayo, washiriki hupata maandalizi na tajriba ya kushiriki katika majukwaa ya kimataifa.”

Kwa mujibu wa Abolqassemi, sifa ya kipekee ya Zayin al-Aswat ni kwamba yanaendeshwa na sekta binafsi. “Sifa hii huwapa waandaaji wa mashindano ujasiri na uhuru wa kuandaa tukio kubwa la Qur'an bila kukumbwa na miundo ya jadi, na kuwa na uwezo wa kubuni mifumo mipya na ya ubunifu kwa ajili ya mashindano.”

Alisema kuwa kuna uwezekano wa kuboresha kwa kiwango kikubwa ubora wa mashindano kwa njia hii. “Tuna mapendekezo mahsusi ya kutekeleza maono haya, na tunatumaini kuwa kwa ushirikiano wa taasisi husika, tutashuhudia mashindano haya yakithibitishwa rasmi katika kalenda ya shughuli za Qur'ani nchini.”

Abolqassemi pia alisisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kuendeleza mashindano kama haya, akisema: “Iwapo vyombo vya habari vitatoa taswira ya kweli ya juhudi za Qur'ani kwa kutumia lugha ya sanaa, hisia, na utaalamu, basi motisha ya kizazi kipya kuingia katika njia hii itaongezeka kwa kiwango kikubwa.”

“Upeperushaji wa moja kwa moja wa usomaji, uchapishaji wa makala fupi kuhusu maisha ya wasomaji vijana, unaweza kuacha athari ya kudumu katika fikra za jamii na kuileta Qur'ani kutoka katika miduara maalum hadi katika nyoyo za watu.”

 

3494903

captcha