
Kampeni hii, inayojulikana kwa jina “Save the Prisoners”, imezinduliwa rasmi ili kuibua uelewa wa dunia kuhusu mateso yanayowakumba maelfu ya wafungwa wa Kipalestina na kuimarisha mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya haki yao.
Waandalizi, katika taarifa ya uzinduzi Jumatano, walisema kampeni inalenga kupanua wigo wa mshikamano na kupeleka kilio cha wafungwa wa Kipalestina mbele ya dhamiri ya dunia, wakikitaja kama moja ya masuala ya dharura na ya kibinadamu kwa wakati huu.
Miongoni mwa mitandao na mashirika yanayoongoza kampeni hii ni Samidoun: Palestinian Prisoner Solidarity Network pamoja na Palestine Solidarity Campaign (PSC).
Kwa mujibu wa taarifa, wafungwa wa Kipalestina wanakabiliwa na hali ngumu na zisizo za kibinadamu, ikiwemo mateso, kutengwa kwa muda mrefu, kunyimwa huduma za afya na ziara za kifamilia, kufungwa bila mashitaka rasmi, pamoja na wanawake na watoto kuwekwa gerezani katika mazingira ya kudhalilisha yanayokiuka sheria na mikataba ya kimataifa.
Kampeni ya miezi sita imepangwa kuunganisha juhudi za kisheria, kibinadamu na kihabari katika nyanja za Kiarabu na kimataifa. Malengo yake ni kufichua uhalifu wa mfumo dhidi ya wafungwa, kushinikiza maboresho ya hali za kifungo, na kudai kukomeshwa kwa sera za mateso na kutengwa.
Aidha, kampeni inasisitiza kuachiliwa kwa dharura wanawake na watoto walioko magerezani, ikibainisha kuwa kulinda heshima ya binadamu ni haki ya msingi isiyoweza kuzuiliwa kwa muda wowote.
Waandalizi wamesema kampeni hii si ishara ya muda mfupi ya mshikamano bali ni jukumu la kimaadili na kibinadamu. Wameeleza kuwa ujumbe wake ni wa kina na wa kimataifa, ukionesha kuwa taabu ya wafungwa imefungamana moja kwa moja na mapambano ya taifa zima linalotafuta uhuru na haki.
Kampeni imewaalika mashirika ya haki za binadamu, vyombo vya habari, asasi za kiraia, wanaharakati wa mitandao ya kijamii na kila mtu mwenye dhamiri ya haki kushiriki kikamilifu katika juhudi hizi.
Lengo kuu ni kuhakikisha kilio cha wafungwa kinabaki mbele ya mijadala ya dunia hadi kila mfungwa apate uhuru kamili na usio na masharti.
Ripoti zinaonyesha kuwa hali za magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel zinatia wasiwasi mkubwa, zikiwa na usafi duni na mateso ya kudumu. Wafungwa wa Kipalestina mara kwa mara wamefanya migomo ya kula kwa muda mrefu kama njia ya kupinga kifungo kisicho cha haki.
Mashirika ya haki za binadamu yameendelea kuripoti kuwa Israel inaendeleza uvunjaji wa haki na uhuru wa wafungwa kinyume na Mkataba wa Nne wa Geneva na sheria za kimataifa.
3496008