IQNA

Jinai za Israel

Utawala wa Israel umeua wanahabari 55 wa Kipalestina tangu 2000

19:38 - January 11, 2023
Habari ID: 3476384
TEHRAN (IQNA) - Waandishi habari wapatao hamsini na watano wa Kipalestina wameuawa na utawala katili wa Israel tangu mwaka 2000 ikiwa ni katika njama za utawala huo wa kikoloni za kuzuia habari za jinai zake dhidi ya Wapalestina kuwafikia walimwengu.

Waandishi hamsini na watano wameuawa, ima kwa kupigwa risasi au kwa kudondoshewa mabomu na Israel tangu mwaka 2000," Naser Abu Baker, Mkuu wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Palestina (PJS), aliuambia mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Ramallah wa Ukingo wa Magharibi.

Aliongeza kuwa waandishi wa habari wawili waliuawa na vikosi vya Israeli mnamo 2022, akiwemo mwandishi wa habari wa Al Jazeera, Shireen Abu Akleh.

Abu Akleh, 51, mwandishi wa habari Mpalestina - Marekani, aliuawa tarehe 11 Mei, ambapo Wizara ya Afya ya Palestina ilisema alipigwa risasi kichwani alipokuwa akiripoti uvamizi wa jeshi la Israel katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin. Jeshi la  utawala dhalimu wa Israel, hata hivyo, lilisema mwandishi huyo huenda aliuawa kwa  risasi "kimakosa" na mwanajeshi wa Israel.

Vyombo kadhaa vya habari duniani, ikiwa ni pamoja na Al Jazeera, CNN, Associated Press, Washington Post na New York Times vilifanya uchunguzi huru, ambao wote walifikia hitimisho kwamba Abu Akleh aliuawa kwa makusudi kwa  risasi ya mwanajeshi wa Israel.

Abu Baker amesema idadi kubwa zaidi ya mashambulizi ya Israel dhidi ya waandishi wa habari wa Palestina imeripotiwa huko al-Quds (Jerusalem).

Aliongoza kuwa mashambulizi haya ya utawala haramu Israel dhidi ya wanahabari  yanalenga kuwazuia kuwafikishia walimwengu ukweli kuhusu maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo yanavyohujumiwa na utawala huo dhalimu.

Abu Baker alisema PJS inachukua hatua kupeleka mashambulizi ya Israel dhidi ya waandishi wa habari kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), bila kutoa maelezo zaidi.

Mohammad Al-Lahham, Mkuu wa Kamati ya Uhuru ya PJS, alisema waandishi wa habari 40 wa Kipalestina walizuiliwa na Wanajeshi wa Israel mwaka jana, 20 kati yao bado wako gerezani.

Hakukuwa na maoni yoyote kutoka kwa utawala dhalimu wa Israeli juu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wapalestina, wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina 224 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza mwaka jana.

3482025

captcha