Katika taarifa ya Jumatano, CPJ ilisema kwamba mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa vifo vingi zaidi tangu kuanzishwa kwa shirika hilo, huku waandishi wa habari 124 wakipoteza maisha kote duniani. Kuongezeka kwa vifo kwa kiwango cha asilimia 22 kutoka mwaka 2023 kulitokana zaidi na vita vya utawala wa Israeli dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, CPJ ilisema.
Waandishi wa habari 85 walikufa wakati wa vita vya miezi 15 katika Gaza, wote wakiuawa mikononi mwa majeshi ya utawala wa Israeli, CPJ ilisema. Waandishi 82 kati ya waliouawa katika kipindi hicho walikuwa Wapalestina.
“Leo ni wakati hatari zaidi kuwa mwandishi wa habari katika historia ya CPJ,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ, Jodie Ginsberg.
“Vita vya Gaza ni vya kipekee katika athari zake kwa waandishi wa habari na inaonyesha kudorora kwa haraka kwa kanuni za kimataifa za kulinda waandishi wa habari katika maeneo ya vita,” aliongeza.
“Katika Gaza na Lebanon, CPJ ilirekodi ... visa ambavyo waandishi wa habari waliuawa na jeshi la Israeli, kinyume na sheria za kimataifa zinazowatambua waandishi wa habari kama raia katika vita,” alisema.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza inasema kuwa idadi ya waandishi wa habari waliouawa na utawala wa Israeli ni kubwa zaidi kuliko takwimu za CPJ.
Kulingana na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Gaza, utawala wa Israeli umewaua waandishi wa habari wasiopungua 205 katika Gaza pekee tangu Oktoba 7, 2023.
Mkataba wa kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa ulianza kutumika Gaza mnamo Januari 19, hatahivyo utawala wa Israel, ukipata himaya kamili ya Marekani, umekuwa ukikiuka mapatano hayo karibu kila siku.
Vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza vimeua angalau Wapalestina 46,707 na kuwajeruhi 110,265 tangu Oktoba 7, 2023. Vita hivyo vimeacha athari kubwa ya uharibifu, na maisha ya zaidi ya Wapalestina milioni mbili yamevurugika kikamilifu.
3491847