IQNA

"Ensaiklopidia ya Usomaji wa Qur’ani”, hatua muhimu ya kuingiza mfumo wa kidijitali katika Sayansi za Qur’ani

15:49 - January 26, 2026
Habari ID: 3481848
IQNA – Ensaiklopidia Maalumu ya Usomaji wa Qur’ani na Sayansi Zake imezinduliwa na Qatar kama kazi mpya inayolinda uhalisia wa kielimu huku ikileta urithi wa qira’ah katika muundo wa kidijitali kwa watafiti na wapenda taaluma za Qur’ani.

Wizara ya Awqaf na Mambo ya Kiislamu ya Qatar imezindua ensaiklopidia hiyo kupitia tovuti ya Islamweb, hatua muhimu inayoongeza uwepo wa sayansi za Qur’ani katika majukwaa ya kidijitali, jambo linaloendana na mwelekeo wa ulimwengu wa Kiislamu unaolenga kuhifadhi turathi kwa njia zinazowafikia vijana na wasomi wa zama hizi.

Katika taarifa yake, wizara ilibainisha kuwa kazi hii imeandaliwa, kukusanywa na kuhaririwa na Sheikh Ahmed Issa Al‑Masrawi, aliyewahi kuwa Sheikh-ul-Qurra wa Misri, mmoja wa magwiji wanaoheshimiwa sana katika ulimwengu wa qira’ah.

Kwa kuwa ni rejea ya kina ya kielimu, ensaiklopidia hii inawasilisha taaluma mahsusi ya usomaji wa Qur’ani kwa mtazamo wa kisasa na wa kimfumo, ikijibu mahitaji ya wanazuoni, wanafunzi na wapenda Qur’ani Tukufu katika ngazi zote.

Chanzo cha ensaiklopidia hii ni ukweli uliothibitishwa na wanazuoni kwamba qirā’āt za Qur’ani ni nyingi, na zote ni njia sahihi za kutamka maneno ya Qur’ani zilizopokelewa kupitia riwaya sahihi kutoka kwa Mtume Mtukufu (SAW). Wanazuoni wamekubaliana juu ya misingi na kanuni zake, na wanazitambua qirā’āt zote sahihi kuwa ni halali kusomwa, kama ilivyoainishwa katika vitabu vinavyoaminika vya elimu ya qirā’āt.

Kazi hii inaunganisha riwaya na utaalamu katika muundo ulio tulivu na wenye mizani, ikilenga kurahisisha maarifa ya kielimu kwa wanaoanza bila kuwapunguzia wataalamu kina cha kielimu wanachokihitaji. Pia inakusanya, kupanga na kuwasilisha maarifa haya katika mfumo wa kidijitali ulio mpangilio mzuri unaorahisisha upatikanaji wake.

Ensaiklopidia ya Usomaji wa Qur’ani na Sayansi Zake inategemea mbinu makini za utafiti wa kielimu, ikinufaika na juhudi na uzoefu wa wanazuoni wa qirā’ah, hasa Sheikh Ahmad Isa al‑Masrawi, ambaye ujuzi wake mpana na wa miaka mingi umeutajirisha mradi huu na kuuboresha mtazamo wake wa kisayansi.

Kwa lengo la kutoa rejea madhubuti inayochanganya uhalisia na mbinu za kielimu, kitabu hiki kinachambua kwa upana elimu ya qirā’āt za Qur’ani. Ensaiklopidia inaanza kwa kuwatambulisha waanzilishi wa qirā’āt kumi rasmi, waratibu wao (ruwāt), pamoja na misururu yao ya isnād isiyokatika.

Baada ya hapo, inafafanua misingi na tofauti zake, inaeleza mbinu za upokezi, na inashughulikia masuala makubwa ya kielimu yanayohusiana na qirā’āt, ikiwemo tofauti kati ya sab‘ah (njia saba za usomaji) na qirā’āt rasmi, pamoja na riwaya zinazotumika zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ensaiklopidia hii inalenga pia kurahisisha na kuikaribisha zaidi elimu ya qirā’āt za Qur’ani, ili wanafunzi na taasisi za kielimu waweze kupata maarifa sahihi na ya kuaminika katika sehemu moja. Hatua hii inachangia kuhifadhi na kutunza turathi ya Kiislamu ya usomaji wa Qur’ani katika mfumo wa kidijitali, sambamba na mwendo wa kasi wa maendeleo ya teknolojia katika kusambaza elimu.

Habari inayofanana:

Aidha, inafanya kazi kama jukwaa wazi la kielimu linaloweza kuunga mkono tafiti za kitaaluma, durusu za kuhifadhi Qur’ani, pamoja na utafiti maalumu wa wanazuoni wanaojikita katika taaluma za qirā’āt.

Ensaiklopidia hii inashughulikia mada pana ndani ya taaluma ya qirā’āt, ikieleza mbinu za usomaji, misururu ya upokezi (asānīd), kanuni za tajwīd, pamoja na tofauti zinazojitokeza kati ya qirā’āt mbalimbali. Aidha, inajumuisha sharh na maelezo ya vitabu vinavyochukuliwa kuwa ruwaza katika elimu ya usomaji wa Qur’ani, sambamba na uthibitishaji wa kielimu kuhusu vyanzo na misingi ambayo taaluma hii imeitegemea kwa karne nyingi.

Kazi hii imesifiwa na wanazuoni na wadau mbalimbali wa sayansi za Qur’ani, ambao wanaiona kama nyongeza yenye thamani kubwa katika majukwaa ya Qur’ani ya mtandaoni, na mchango muhimu katika kuendeleza utafiti wa kisayansi katika nyanja ya qirā’āt.

4330043

captcha