IQNA

Vituo 14 kuwahudumia Watoto katika mafunzo ya asubuhi ya Qur'ani majira ya kiangazi nchini Qatar

20:27 - July 15, 2025
Habari ID: 3480947
IQNA – Mafunzo ya Qur'ani ya asubuhi wakati wa kiangazi yanatarajiwa kufanyika katika vituo 14 vya Qur'ani kote nchini Qatar kuanzia Jumapili.

Idara ya Da’wah na Mwongozo wa Kidini katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar imetangaza kufunguliwa kwa usajili wa mafunzo hayo ya Qur'ani ya asubuhi.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kutumia likizo ya kiangazi kukuza elimu na maadili ya kidini miongoni mwa vijana.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, wizara ilisema kuwa programu hii inalenga wavulana wenye umri wa miaka mitano na kuendelea, na inahusisha mafundisho ya tahajia ya msingi na uhakiki wa usomaji wa Qur’ani Tukufu, sambamba na vipindi vya elimu vitakavyosaidia kukuza maadili ya Kiislamu na mienendo chanya kwa washiriki.

Vipindi hivi vitaanza rasmi Jumapili ijayo asubuhi na vitaendelea hadi mwisho wa mwezi, vikifanyika katika vituo 14 vya Qur’ani vilivyotapakaa maeneo mbalimbali ya nchi, ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kunufaika kwa urahisi.

Mafunzo yatakuwa yakifanyika siku nne kwa wiki, kuanzia Jumapili hadi Jumatano, kati ya saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, chini ya usimamizi wa walimu waliobobea katika ufundishaji wa Qur’ani na elimu zake.

Idara ya Da’wah na Mwongozo wa Kidini imesisitiza umuhimu wa programu hizi katika kuwalea watoto wapende Qur’ani Tukufu na kuimarisha maadili ya Kiislamu katika mazingira salama na yenye kuchochea elimu.

Mpango huu ni sehemu ya mkakati wa wizara wa kusambaza elimu ya Kiislamu na kuongeza uelewa wa kidini katika jamii, hasa miongoni mwa vijana.

Hatua hii itachangia katika kulea kizazi chenye ufahamu, kinachoshikamana na utambulisho wake wa Kiislamu.

3493852

Kishikizo: qatar qurani tukufu
captcha