IQNA

Wanafunzi wa Qatar washiriki kozi ya Majira ya Joto ya Kuhifadhi Qur'ani

14:10 - July 25, 2025
Habari ID: 3480998
IQNA – Wanafunzi thelathini wa Qatar wameshiriki katika kozi ya majira ya joto ya wiki tatu iliyoandaliwa na Kituo cha Elimu ya Qur'ani cha Al Noor kwa lengo la kuboresha kuhifadhi Qur'ani Tukufu na kukuza ujuzi wa kielimu.

Kozi hii ya kwanza ya kiangazi imeandaliwa na Kituo cha Elimu ya Qur'ani cha Al Noor, ambacho kipo chini ya Idara ya Da’wa na Mwongozo wa Kidini katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar.

Mpango huu wa wiki tatu ulibuniwa kuwasaidia wanafunzi kuimarisha uhifadhi wao wa Qur'ani Tukufu sambamba na kukuza uwezo wao wa kielimu na kitaaluma wakati wa mapumziko ya kiangazi, kwa mujibu wa ripoti ya Qatar Tribune iliyotolewa Jumatano.

Kama sehemu ya ratiba, kila mwanafunzi alitarajiwa kuhifadhi kurasa mbili za Qur’ani kila siku pamoja na kupitia sehemu walizokwisha zihifadhi hapo awali.

Kozi hii ni sehemu ya mfumo mpana wa elimu unaojumuisha masomo ya misingi ya Qur’ani, ibada za vitendo, mafunzo ya sauti (makhraj na tajweed), shughuli za mwili, na matembezi ya elimu na burudani.

Mbali na masomo ya dini, wanafunzi walihudhuria pia vipindi vya taaluma mbalimbali kama vile usalama wa mitandao (cybersecurity). Aidha, programu ilihusisha warsha za kaswida (chanting) na mafunzo ya kutoa Adhana (mwito wa swala).

3493972

Kishikizo: qatar qurani tukufu
captcha