
Msikiti huu unatambulika pia kama kituo mashuhuri cha elimu, kutokana na kuwepo kwa maktaba kubwa inayohifadhi mamia ya vitabu muhimu vya Kiislamu, vinavyohudumia wanazuoni, watafiti na wanafunzi wa elimu ya dini.
Jiji la Kuwait, lililopo katika mwambao wa kaskazini-magharibi mwa Ghuba ya Uajemi, lina hazina ya athari na majengo ya kihistoria yanayovutia wageni na watalii wa ladha mbalimbali. Miongoni mwa vivutio hivyo ni Msikiti Mkuu wa Kuwait, unaochukua nafasi ya kipekee katika urithi wa taifa hilo.
Kama mmoja kati ya misikiti mikubwa zaidi duniani, Msikiti Mkuu wa Kuwait ulichorwa na msanifu majengo mashuhuri Mohammed Saleh Makiya, kwa mchanganyiko wa mitindo ya Andalusia na Mashariki, kwa kuzingatia turathi za usanifu wa jadi wa Kiislamu. Alama za usanifu wa Kiarabu zinajitokeza wazi katika kuta zake, zikitoa taswira ya uhalisia wa sanaa ya Kiislamu ya kale na ya kisasa.
Ujenzi wa msikiti huu ulianza mwaka 1979, kwa ushiriki wa wahandisi 50 na zaidi ya wafanyakazi 400, kwa gharama inayokadiriwa kufikia dola milioni 45 za Marekani. Msikiti ulifunguliwa rasmi mwaka 1987, na tangu hapo umekuwa kivutio kikubwa cha ibada, ukipokea idadi kubwa ya waumini wa kiume na wa kike. Kwa ujumla, eneo lake lina uwezo wa kuchukua zaidi ya waumini 60,000.

Kwa mujibu wa Ali Shaddad, Mkurugenzi wa Msikiti Mkuu wa Kuwait, eneo la msikiti linakadiriwa kuwa takribani mita za mraba 45,000. Ukumbi mkuu wa swala una uwezo wa kuchukua waumini 10,000, na kwa kujumlisha viwanja vya nje na baraza zake, idadi hiyo hufikia takribani watu 60,000. Aidha, wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, hasa katika masiku ya Laylatul-Qadr, idadi ya waumini hufikia takribani 150,000, alibainisha.
Shaddad alieleza kuwa mapambo na michoro iliyochongwa katika kuta za msikiti huo ni kazi ya mikono, iliyofanywa kwa uangalifu na juhudi kubwa, yakidhihirisha ustadi wa hali ya juu wa sanaa ya Kiislamu.
Kwa mujibu wake, msikiti upo upande wa kaskazini-mashariki wa Jiji la Kuwait, na eneo lililojengwa lina mita za mraba 24,000, huku sehemu iliyosalia ikitumika kwa ujenzi wa chemchemi za maji na upandaji wa mitende pamoja na mimea mingine inayopamba korido na viunga vya msikiti.
Akizungumzia muundo wa jengo, Shaddad alisema misingi, nguzo, paa na mnara wa msikiti vimejengwa kwa saruji. Nje ya jengo limefunikwa kwa mawe ya asili, ilhali ndani limepambwa kwa marumaru, kauri na plasta, sambamba na michoro ya kijiometri inayoakisi shule za usanifu wa Kiislamu za jadi na za kisasa.
Msikiti Mkuu wa Kuwait si tu fahari ya usanifu na mahali pa ibada lenye heshima, bali pia ni kitovu mashuhuri cha elimu na maarifa. Ndani yake kuna maktaba kubwa yenye mamia ya vitabu vya marejeo ya Kiislamu, vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa shughuli za utafiti na tafakuri ya kielimu. Aidha, msikiti una ukumbi maalumu wa kuandaa semina, mihadhara, na programu mbalimbali za kitamaduni na kielimu.
Kwa hakika, msikiti huu una maktaba mbili kubwa. Maktaba ya kwanza imetengwa kwa wanazuoni na watafiti, na ndani yake kuna nakala adimu ya Qur’ani ya Kiothmania inayohifadhiwa kwa heshima kubwa.
Maktaba ya pili ni ya kimataifa, ikiwa na vitabu katika lugha zisizo za Kiarabu, na imekusudiwa kuwahudumia wasiokuwa Waislamu pamoja na wasomaji wasiozungumza Kiarabu, ikiwa ni daraja la maelewano, elimu na mawasiliano baina ya tamaduni.
4323172