IQNA

Shughuli za Qur'ani

Wanafunzi kutoka Nchi 52 Wanufaika na Mipango ya Jumuiya ya Qur’ani ya Kuwait

11:41 - July 27, 2022
Habari ID: 3475546
TEHRAN (IQNA) – Wanafunzi wa shule katika nchi 52 hadi sasa wamenufaika kutokana na shughuli za jumuiya ya Qur’ani ya Kuwait ambayo inatoa misaada ya kimaisha na huduma za Qur’ani katika sehemu mbalimbali za dunia.

Jumuiya ya Kutumikia Qur’ani na Sayansi Zake ilianzishwa nchini Kuwait mnamo 2016 ili kutumikia Kitabu Kitakatifu, kukuza uhusiano wa kistaarabu na kitamaduni na Waislamu, haswa waliosilimu, kote ulimwenguni, kuzindua vituo vya kuhifadhi Qur'ani, na shughuli zingine.

Kulingana na jumuiya hii, shughuli zake hadi sasa zimesaidia wanafunzi wa shule 31,000 katika nchi 52, ikiwa ni pamoja na Chad, Mauritania, Syria, Niger na Ghana.

Programu za jumuiya hiyo ni pamoja na kutuma nakala za Qur’ani zenye tafsiri katika lugha tofauti, kufanya duru za Qur'ani, kuwezesha safari za Hija kwa baadhi ya Waislamu wa Asia Kusini, kuwasaidia wakimbizi wa Syria, kutekeleza mipango mbalimbali ya kutoa misaada, na kusambaza nyama kwa maskini katika nchi 13 wakati wa Idul Adha.

Pia huandaa mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu kwa lengo la kukuza shughuli za Qur'ani za Kuwait.

Jumuiya hiyo inatumai itaendeleza shughuli zake kwa Waislamu waliosilimu barani Ulaya, Marekani na Amerika Kusini katika siku za usoni.

Maafisa wake wanasema Waislamu waliosilimu karibuni katika maeneo hayo wanahitaji tafsiri za Qur’ani katika lugha zao ili kuelewa vyema mafundisho ya Kitabu hicho Kitakatifu.

Pia kuna haja ya mipango katika nchi za Magharibi kukabiliana na chuki dhidi Uislamu, maafisa wa jamii wanasema.

4073535

Kishikizo: kuwait qurani tukufu
captcha