IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran yatafanyika ana kwa ana ikiwa hali ya usalama itatengamaa

15:26 - July 22, 2026
Habari ID: 3482523
IQNA – Mkuu wa Shirika la Awqaf na Mambo ya Hisani la Iran amebainisha kuwa hatua ya fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yatafanyika ana kwa ana, ikiwa tu hali ya usalama itaruhusu kufanyika kwa hafla hiyo kuu.

Katika mkutano uliofanyika Tehran siku ya Jumanne kwa ajili ya kujadili maandalizi ya mashindano ya kitaifa na kimataifa ya Qur'ani, Hujjatul Islami Sayyid Mehdi Khamoushi alisema: “Ikiwa hali itaruhusu, hatua ya mwisho ya Mashindano ya 49 ya Kitaifa ya Qur'ani yatafanyika katika Mkoa wa Sistan na Baluchestan; vinginevyo, Tehran itakuwa mwenyeji. Kuhusu mashindano ya kimataifa, yatafanyika ana kwa ana au kwa njia ya mtandao, kulingana na hali ya usalama nchini.”

Kauli hii ya Hujjatul Islam Khamoushi inaashiria tahadhari ya kiusalama inayotokana na mazingira ya vita na uchokozi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hujjatul Islam Khamoushi alikumbusha kuwa wakati wa janga la korona, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa nchi pekee iliyoweza kufanikisha mashindano yake ya kimataifa ya Qur'ani bila kusitishwa, ambapo yaliendeshwa kwa njia ya kidijitali (virtual).

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'an Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo huandaliwa kila mwaka na Shirika la Awqaf na Mambo ya Hisani, ni nguzo muhimu katika kueneza utamaduni na thamani za Qur;ani miongoni mwa Ummah wa Kiislamu, huku yakitoa fursa ya kuibua na kuenzi vipaji vya wasomaji na wahifadhi wa Kitabu Kitukufu.

Hatua ya mwisho ya toleo la 42 la mashindano haya inatarajiwa kufanyika kwa ushiriki wa wawakilishi kutoka nchi 58 duniani kote, jambo linalodhihirisha nafasi ya kipekee ya Iran kama kitovu cha elimu na usomaji wa Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu.

3498370

captcha