IQNA

Arbaeen ni fursa ya kipekee ya kueneza utamaduni wa Qur’ani

16:03 - July 21, 2026
Habari ID: 3482521
IQNA – Mkuu wa Makao Makuu ya Kati ya Arbaeen nchini Iran amesisitiza umuhimu wa matembezi ya kila mwaka ya Arbaeen kama fursa adhimu ya kueneza utamaduni wa Qur’ani.

Ali Akbar Pourjamshidian pia amesema kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Qur’ani wa ‘Kuishi na Aya’ Iran katika hafla hii kuu unaweza kuweka msingi kwa mamilioni ya mazuwaru kupata ufahamu zaidi na kuzama katika mafundisho ya Qur’ani Tukufu.

Ameyasema hayo siku ya Jumatatu, Julai 19, wakati wa sherehe za utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Makao Makuu ya Kati ya Arbaeen na Shirika la Dar-ol-Quran al-Karim.

Pourjamshidian ametoa shukrani zake kwa shughuli za Qur’ani na utamaduni zinazofanyika nchini humo na kusema, “Katika miezi ya hivi karibuni, tumeshuhudia uzalishaji wa maudhui mafupi, ya kina na yenye ufanisi katika nyanja ya utamaduni na Qur’ani; mfano mzuri wa mafanikio hayo ulihusishwa katika programu za kiutamaduni za hafla za kuwazungumzia mashahidi wa hivi karibuni wa nchi yetu.”

Ameongeza, “Uteuzi wa nembo zinazofaa, uzalishaji wa maudhui bora, na matumizi ya alama za kiutamaduni katika hafla hizo yalikuwa na mwitikio nje ya mipaka ya Iran na kuvutia umakini wa ulimwengu. Uzoefu huu wa thamani unapaswa pia kuzingatiwa katika programu za kiutamaduni za Arbaeen.”

Akisisitiza kuwa Arbaeen haipaswi kuchukuliwa kama hafla ya Iran pekee, amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sehemu tu ya vuguvugu hili kubwa la kimataifa, na mipango ya kiutamaduni ya Arbaeen inapaswa kufanywa kwa mtazamo huo mpana.

Amesema kuwa hata uteuzi wa nembo ya Arbaeen unafanywa kwa ushiriki na maafikiano ya vikundi vya kitamaduni kutoka nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Iraq, Lebanon, Marjaa’i (mamlaka kuu za wanazuoni wa Kishia), na wanaharakati wengine wa Mhimili wa Muqawama, na hii inaashiria asili ya kimataifa ya vuguvugu hili kubwa.

Amesisitiza tena uwezo wa kiutamaduni wa matembezi ya Arbaeen na kusema kuwa njia ya kutembea ya Arbaeen ni fursa bora zaidi kwa mazuwaru kupata ufahamu zaidi kuhusu Qur’ani.

“…kwa mipango mizuri, mazuwaru wanaweza kuhimizwa kuhifadhi na kutafakari aya za Qur’ani.”

Ameendelea kusema kuwa hata kuhifadhi Sura fupi au aya chache katika njia ya kutembea kunaweza kuwa na athari kubwa katika uhusiano wa mazuwaru na Qur’ani, na jambo hili linawezekana kabisa kwa kubuni programu za motisha na kiutamaduni.

Arbaeen ni maadhimisho matukufu ya kidini yanayofanywa na Waislamu, hususan wa madhehebu ya Shia, katika siku ya arubaini baada ya Siku ya Ashura, kuadhimisha kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Waislamu wa madhehebu a Shia.

Hii ni moja ya ziyara kubwa zaidi za kila mwaka ulimwenguni, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Shia, pamoja na idadi kubwa ya Masunni na wafuasi wa dini nyinginezo, hutembea kwa miguu kuelekea mji mtukufu wa Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen inasadifia tarehe 4 Agosti.

3498351

Kishikizo: iran arbaeen
captcha