Baada ya hafla zisizo na mfano wake huko Tehran, Qom, Najaf na Karbala, msafara wa mazishi uliwasili kwenye kituo chake cha mwisho mjini Mashhad, ambako mwili ulipokelewa na umati mkubwa wa waombolezaji kutoka kila pembe ya Iran na kutoka makumi ya nchi mbalimbali duniani, kabla ya kuzikwa kandokando ya haram hiyo tukufu siku ya Alhamisi.
Mamilioni ya waombolezaji, waliokuwa wamekusanyika tangu asubuhi na mapema, waliandamana na gari lililobeba miili hiyo yenye baraka, na hivyo kuigeuza miji na mitaa ya Mashhad kuwa mandhari ya adhama, heshima na mapenzi ya kipekee.
Ukubwa wa mkusanyiko huo ulikuwa wa aina ambayo ni vigumu kuelezeka. Tangu wakati gari la mazishi lilipoingia Mtaa wa Imam Ridha, lilizungukwa kabisa na mawimbi ya waombolezaji waliowasili kutoka kila kona ya Iran, Wakurdi, Waturuki, Waajemi, Waarabu na Walur,wote wakiwa wameungana katika huzuni na azma.
Nyuso zao zilizolowa machozi na nara zao zenye hamasa zilijaza anga, na kuunda hali ambayo mashuhuda waliitaja kuwa ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya umoja wa kitaifa katika historia ya hivi karibuni.
Nara za “Mauti kwa Marekani,” “Mauti kwa Israel,” na “Mauti kwa wanaoupinga Wilayatul Faqih” zilisikika katika njia nzima ya msafara, zikidhihirisha mshikamano usioyumba wa wananchi kwa misingi ambayo kiongozi huyo shahidi aliitetea katika maisha yake yote.
Bendera nyekundu za kulipiza kisasi zenye maandishi “Ya Latharat al-Husayn” na mabango ya Jamhuri ya Kiislamu yalitanda katika mitaa mbalimbali, yakibeba alama ya maombolezo pamoja na azma ya kutafuta haki.
Miongoni mwa waombolezaji, msisitizo maalumu ulionekana kwa ujumbe kutoka makabila na jamii mbalimbali. Waislamu wa Kisunni kutoka Sistan na Baluchestan, waliovalia mavazi yao ya jadi ya rangi nyeupe, walionekana waziwazi baada ya kusafiri hadi Mashhad kwa ajili ya kutoa heshima zao.
Wawakilishi kutoka mkoa wa Chaharmahal na Bakhtiari, waliovalia mavazi yao mahsusi ya jadi, waliinua juu bendera ya taifa katikati ya umati.
Uwepo wa makundi hayo tofauti ulikuwa ushahidi madhubuti wa tabia jumuishi ya turathi za marehemu kiongozi na mafungamano ya ndani ya umoja aliyoyakuza baina ya tabaka zote za jamii ya Kiirani.
Umuhimu wa tukio hilo haukuishia ndani ya mipaka ya Iran pekee. Waombolezaji kutoka Afghanistan, Pakistan, India, Uturuki, Nigeria, Tanzania na Kenya walivuka mipaka ya kijiografia ili kutangaza kwamba ujumbe wa kupinga uistikbari, kulinda heshima, uhuru na izza uliotetewa na kiongozi huyo shahidi umevuka mipaka na kugusa nyoyo za wengi kote duniani.
Wakati wa kuhuzunisha zaidi ulijitokeza pale mwombolezaji mmoja kutoka Canada, aliyesafiri zaidi ya kilomita 10,000 ili kuhudhuria, alipozungumzia heshima yake kubwa kwa mtu ambaye, kwa mujibu wake, athari yake ilizidi mipaka ya taifa lolote moja.
Vivyo hivyo, mwombolezaji mmoja kutoka India alieleza jinsi habari ya kuuawa Shahidi Imam Khamenei ilivyovunja nyoyo za Waislamu katika bara dogo la Hindi, na kuwafanya wafike Mashhad kushiriki katika kuaga huku kwa kihistoria.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, pia alikuwepo miongoni mwa waombolezaji; ushiriki wake ukisisitiza mvumo wa kimataifa wa ujumbe wa Kiongozi Shahidi wa kusimama dhidi ya dhulma na uonevu.
Waombolezaji kutoka Uturuki waliskika wakipaza nara “Labbaik Ya Sayyid Mojtaba” kwa nia ya kutangaza utiifu wao kwa Kiongozi Muadhamu aliyechaguliwa, Ayatullah Mojtaba Khamenei. Aidha waombolezaji kutoka Nigeria walitoa nara kama hiyo na kuonyesha utiifu wao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Wakati mmoja, msongamano mkubwa wa watu uliilazimisha gari la mazishi kubadili njia kutoka Makutano ya Danesh, na kuelekezwa upande wa uwanja wa mpira wa Ferdowsi, ambako helikopta ilitumika kubeba miili hiyo yenye baraka hadi kwenye haram.
Katika msafara wote, sauti ya Kiongozi huyo Shahidi ilisikika kupitia vipaza sauti, jambo ililosababisha mawimbi ya vilio vya pamoja kusambaa katika umati mkubwa wa watu.
Mabango yenye ujumbe wa Kiingereza yaliyosomeka “We stand up to the end…” yalionekana miongoni mwa umati, yakionesha azma ya wananchi ya kuendeleza njia ya muqawama.
Swala ya maiti iliongozwa na mwana mkubwa wa kiongozi huyo shahidi, Sayyid Mostafa Khamenei, ambaye aliswalisha ibada hiyo juu ya miili hiyo.
Umati ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba mbali na eneo la haram yenyewe, swala pia ilisaliwa katika mitaa ya Navvab Safavi, Tabarsi na Shirazi, ambako waombolezaji wengi walikuwa wamekusanyika.
Kiongozi huyo shahidi pamoja na baadhi ya wanafamilia wake waliuawa kishahidi katika shambulio la kigaidi la tarehe 9 Machi, lililotekelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya makazi ya kiongozi huyo.
Miongoni mwa waliouawa sHAHIDI walikuwemo mke wa Kiongozi mpya Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, mkwe wa kiongozi marehemu; binti wa marehemu kiongozi; pamoja na mjukuu wake wa kike mwenye umri wa miezi 14.
Shughuli za mazishi zilianza Ijumaa iliyopita, zikiambatana na salamu za pole na heshima kutoka kwa maafisa wa kisiasa na wanazuoni kutoka zaidi ya nchi 90. Hilo lilifuatiwa na hafla za kuaga katika Musalla wa Tehran mwishoni mwa juma, ambako mamilioni walifika kutoa heshima zao.
Siku ya Jumatatu, miili ilipitishwa katika mji wa Tehran kwa ushiriki mkubwa wa halaiki, na siku ya Jumanne hafla zikafanyika mjini Qom na katika Msikiti wa Jamkaran.
Ushiriki huo mkubwa uliendelea kimataifa pia, pale takribani Wairaq milioni 10 walipokusanyika Najaf na Karbala siku ya Jumatano kutoa heshima zao.
Maafisa wa Iraq walithibitisha kwamba huo ulikuwa miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya mazishi katika historia ya karibuni. Viongozi wa kidini na kisiasa kote Iraq walishiriki katika hafla hizo, wakionesha mafungamano ya kina baina ya watu wa Iran na Iraq yaliyojengwa juu ya imani ya pamoja na mapambano ya pamoja.
Hatimaye, msafara wa mazishi ulipohitimishwa kwa maziko ndani ya ukumbi wa swala wa Dar al-Dhikr, ulioko karibu na Rawdhah tukufu na kandokando ya ukumbi wa swala wa Dar al-Surur katika ua wa Azadi wa haram hiyo, siku hiyo itakumbukwa kama moja ya siku zenye uzito mkubwa zaidi katika historia ya kisasa ya Iran.
Mahali hapo palichaguliwa ili kurahisisha upatikanaji kwa mahujaji watakaokuja baadaye kutoa heshima zao.
Uwepo wa waombolezaji waliobeba mabango yanayomlaani Rais wa Marekani Donald Trump na kupaza nara za kutaka kisasi, uliakisi msimamo wa wananchi wa kusisitiza kuwawajibisha wahusika wa jinai hiyo.
“Muuaji wa kiongozi hastahili isipokuwa kitanzi / Hakutakuwa na msamaha,” walipaza sauti, huku wengine wakitaka “Kisasi, kisasi” kutoka kwa vikosi vya ulinzi.
Hata usiku ulipoingia na hafla rasmi kuhitimika, makundi ya watu yaliendelea kukusanyika katika mitaa inayozunguka haram, yakisoma dua na kuonesha mapenzi yao.
Bendera nyekundu na nyeusi za maombolezo na kulipiza haki ziliendelea kupepea, huku kauli “Labbaik Ya Hussein” zikisikika katika mitaa, na hivyo kuhakikisha kwamba roho ya kuaga huku kwa kihistoria inaendelea kubaki hai hata baada ya msafara wenyewe kumalizika.
Maonesho haya yasiyo na mfano ya umoja wa kitaifa na mshikamano wa kimataifa hayakuheshimu tu kumbukumbu ya kiongozi mpendwa, bali pia yamedhihirisha upya msimamo usioyumba wa taifa la Iran kwa misingi ya uhuru, muqawama dhidi ya dhulma, na uaminifu kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Shahidi amepata mahali pake pa mapumziko ya milele, lakini turathi zake na azma ya wafuasi wake ya kuendeleza njia yake vinaendelea kuwa hai na vyenye nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
3498181