IQNA – Kituo cha Dar-ol-Quran cha Atabat au Mfawidhi wa haram takatifu ya Imam Hussein (AS) kimekamilisha mradi wa vituo vya Qur’ani kwa ajili ya matembezi ya Arbaeen.
Mpango huu ulitekelezwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Vyuo vya Kiislamu cha Najaf wakati wa kipindi chote cha Ziyara ya Arbaeen. Vituo hivi vya Qur’ani vilivyowekwa kama sehemu ya mpango huu vilitoa huduma kwa maelfu ya Mazuwar.
Mradi huu uliwahudumia zaidi ya watu 81,000, na programu zake zilifanyika kwa ushiriki wa walimu 750 wa Qur’ani, wanaume kwa wanawake, waliokuwa wakiendesha shughuli zao katika vituo 90 vilivyosambaa katika mkoa wa Karbala na mikoa mingine kadhaa nchini Iraq.
Sheikh Khairuddin Al-Hadi, Mkuu wa Kituo cha Dar-ol-Quran, alisema kuwa mapokezi makubwa ya vituo hivi vya Qur’ani yanathibitisha mafanikio ya mradi huu katika kufikisha ujumbe wa Qur’ani kwa Mazuwar.
“Wafanyakazi wa kituo walifanya kazi kwa bidii kwa kipindi cha siku saba ili kuongeza uelewa na kutoa huduma za kielimu na za Qur’ani, ambazo zilisaidia kurekebisha usomaji na kuimarisha uelewa wa kidini na kiutamaduni wa Mazuwar,” alisema.
Al-Hadi aliongeza kuwa mradi huo ulijumuisha shughuli mbalimbali, zikiwemo mikusanyiko saba ya kimataifa ya Qur’ani na mikusanyiko 47 ya ndani.
“Aidha, kituo kiliandaa mashindano na makongamano 23, pamoja na mihadhara 82 ya kuongeza uelewa kuhusu mada mbalimbali za Qur’ani na dini, na kugawa zaidi ya zawadi 25,000 zenye baraka kwa Mazuwar,” aliongeza.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya kila mwaka ya mradi huu ni kichocheo cha kuendeleza na kupanua huduma zake katika fursa zijazo, na yataimarisha utoaji wa programu za Qur’ani kwa wale wote wanaokuja kumzuru Imam Hussein (AS).
Al-Hadi alihitimisha kwa kukumbusha kuwa mradi huu pia unaakisi huduma Atabat katika kueneza utamaduni wa Qur’ani na kuingiza thamani zake katika jamii.
3498566