El-Sayed alimshinda Mwakilishi Haley Stevens, ambaye alikuwa amepokea makumi ya mamilioni ya dola za ufadhili kutoka makundi yanayounga mkono Israel, na ambaye alionekana kuwa mgombea mwenye nafasi kubwa katika uchaguzi mkuu. Ushindi wake umevuta hisia kubwa kutokana na msimamo wake wa kisiasa wa mrengo wa mabadikiko, ikiwemo wito wake wa wazi wa kusitisha misaada ya kijeshi ya Marekani kwa utawala wa Israel.
Kituo cha Israel cha Channel 14 kilieleza matokeo hayo kama ushindi mkubwa kwa 'mrengo wa msimamo mkali wa wapenda mageuzi' ndani ya Chama cha Democratic. Kituo hicho kilisema mafanikio ya El-Sayed yanaweza kuathiri mijadala ya baadaye ndani ya chama hicho, hasa kuhusu sera kuelekea Israel, na yanaweza pia kuchochea mijadala kuelekea uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2028.
Gazeti la Israel Hayom liliutaja ushindi huo kuwa “mafanikio makubwa” kwa mrengo wa wapenda mageusi na “pigo zito” kwa Kamati ya Masuala ya Umma ya Marekani na Israel, inayojulikana kama AIPAC. Kwa mujibu wa gazeti hilo, mrengo wa kisiasa wa AIPAC, United Democracy Project, ulitumia zaidi ya dola milioni 30 kumuunga mkono Stevens na kujaribu kuzuia El-Sayed kupata uteuzi.
Gazeti jingine la Israel, Yedioth Ahronoth, lilimtaja El-Sayed kama “Obama Muislamu,” likisema kuwa ingawa kinyang’anyiro hicho kilikuwa cha ndani katika ngazi ya jimbo, kilionekana kwa upana kama kipimo cha mwelekeo wa baadaye wa Chama cha Democratic, hasa kuelekea uchaguzi wa Bunge la Congress.
Shirika la utangazaji la umma la Israel, KAN, pia lilisema matokeo hayo yanaonyesha ushindani unaoongezeka kati ya mrengo wa 'wastani' na mrengo wa 'wapenda mageuzi' ndani ya Chama cha Democratic kuhusu sera ya Washington kwa Israel. Liliongeza kuwa iwapo El-Sayed atachaguliwa kuwa seneta mwezi Novemba, anaweza kuathiri mijadala na misimamo ya Seneti kuhusu masuala yanayohusiana na Israel.
El-Sayed atakabiliana na aliyekuwa Mwakilishi wa Republican, Mike Rogers, ambaye hakupata mpinzani ndani ya chama chake, katika uchaguzi wa Novemba 3. Kiti hicho kiko wazi baada ya Seneta Gary Peters kutangaza kustaafu, na kinachukuliwa kuwa muhimu kwa matumaini ya Democratic kurejesha udhibiti wa Seneti ya Marekani.
Iwapo atashinda, El-Sayed atakuwa Muislamu wa kwanza kuhudumu katika Seneti ya Marekani. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 41 alizaliwa Rochester Hills, Michigan, kwa wazazi wahamiaji kutoka Misri. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Michigan, akapata shahada ya udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Columbia, na baadaye akatunukiwa shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.
El-Sayed aliwahi kugombea katika kura za mchujo za Democratic za ugavana wa Michigan mwaka 2018, lakini akashindwa na Gretchen Whitmer. Tangu wakati huo, ameibuka kuwa mmoja wa watu mashuhuri katika mrengo wa maendeleo wa Chama cha Democratic.
3498554