Katika mahojiano na Radio Arbaeen, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na ambaye kwa sasa ni mbunge, Manouchehr Mottaki, alisema kuwa Arbaeen ya kwanza baada ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) iliadhimishwa na msafara wa mateka wa Karbala ulioongozwa na Bibi Zainab al-Kubra (SA). Baada ya kustahimili mateso ya utekwa huko Kufa na Damascus, familia ya Mtume Muhammad (SAW), yaani Ahlul-Bayt, ilirejea Karbala katika siku ya arobaini, ambapo Bibi Zainab akawa Zuwar wa kwanza kuzuru Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) baada ya Ashura.
Alibainisha kuwa ziara hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa wa kihisia na kihistoria. Wakati familia ya Mtume (SAW) iliporejea kuomboleza na kuhuisha ahadi yao, Bibi Zainab pia aliendeleza ujumbe wake wa kuamsha ufahamu kupitia hotuba zake, akihakikisha kuwa malengo na ujumbe wa qiyam ya Imam Hussein (AS) vinahifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mottaki alisema kuwa tangu wakati huo, Arbaeen imekuwa nembo ya kudumu ya mapenzi na uaminifu kwa Imam Hussein (AS), na leo hii tukio hilo hushuhudia mkusanyiko mkubwa zaidi wa kila mwaka wa watu duniani.
Akizungumzia ziara ya mwaka huu, alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Iraq, takribani Mazuwar milioni 4.8 Wairani wameshiriki katika matembezi ya Arbaeen, jambo linalodhihirisha ukubwa wa kipekee wa harakati hii.
Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje alisisitiza kuwa harakati ya Ashura inaendelea kuyapa mataifa ilhamu, akisema kuwa matukio ya hivi karibuni yameonesha kwamba ujumbe wa Karbala bado ni chemchemi ya mwamko na uhamasishaji. Aliongeza kuwa taifa la Iran pia limeonesha uthabiti wake kwa kuchota ilhamu kutoka katika utamaduni wa Ashura.
Akinukuu tamko la kihistoria la Imam Hussein (AS), “Mtu kama mimi kamwe hatatoa kiapo cha utii kwa mtu kama, yeye,-yaani Yazid,” Mottaki alisema Imam alikataa kusalimu amri mbele ya dhulma hadi katika dakika yake ya mwisho. Ingawa aliuawa shahidi, jina lake na njia yake vimebaki milele, ilhali Yazid amebaki kukumbukwa katika historia kwa chuki, laana na fedheha.
Akirejea msafara wa mazishi ya Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika miji mitukufu ya Iraq ya Najaf na Karbala, alisema ushiriki mkubwa wa wananchi ulidhihirisha mshikamano wa kina kati ya utamaduni wa kujitolea na shahada na harakati ya Ashura. Aliongeza kuwa njia hii itaendelea kwa nguvu, izza na heshima.
3498536