IQNA

Ujumbe wa Kosovo washinda Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Skopje

15:48 - August 03, 2026
Habari ID: 3482580
IQNA – Wasomaji na mahafidh wa Qur'ani Tukufu kutoka Kosovo wameibuka kuwa ujumbe uliofanya vyema zaidi katika Mashindano ya Nne ya Kimataifa ya Qur'ani ya Balkan yaliyofanyika mjini Skopje, mji mkuu wa Macedonia Kaskazini.

Mashindano hayo ya kimataifa yalifanyika kuanzia Julai 26 hadi 29, yakikusanya takribani washiriki 300 kutoka nchi 29.

Kosovo ilitangazwa kuwa ujumbe bora zaidi baada ya kujinyakulia tuzo 10 kati ya tuzo 30 zilizotolewa katika mashindano hayo.

Licha ya kuwa taifa dogo na lililopata uhuru wake katika kipindi cha karibuni, Kosovo imeendelea kujidhihirisha kama miongoni mwa mifano bora barani Ulaya katika elimu ya Qur'ani Tukufu na malezi ya wasomaji wa Qur'ani. Nchi hiyo, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu kwa mujibu wa mlingano wa idadi ya watu barani Ulaya, ina mfumo wa elimu ya Kiislamu unaosimamiwa na taasisi za kidini zenye mchango mkubwa katika medani za kimataifa za Qur'ani.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Skopje yamekuwa ushahidi mwingine wa mafanikio hayo, baada ya ujumbe wa Kosovo kuongoza orodha ya nchi 29 zilizoshiriki na kupata matokeo bora kwa ujumla. Mafanikio hayo yalitokana na utendaji wa kiwango cha juu wa washiriki wake katika vipengele mbalimbali vya kuhifadhi na kusoma Qur'ani Tukufu.

Hafidh Alban Dali aliongoza orodha ya washindi kwa kutwaa nafasi ya kwanza katika kipengele cha kuhifadhi Qur'ani Tukufu yote, jambo lililokuwa miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi ya mashindano hayo.

Katika kipengele cha kuhifadhi juzuu 10, Samra Bashani alipata nafasi ya pili kwa upande wa wasichana, huku Marigona Mileva na Hana Maloku wakigawana nafasi ya tatu. Katika kuhifadhi juzuu tano, Mehmet Morena alipata nafasi ya tatu kwa upande wa wavulana, naye Darya Smaili akachukua nafasi ya tatu kwa upande wa wasichana.

Katika kipengele cha kuhifadhi juzuu mbili, Emra Shala alishika nafasi ya kwanza kwa wasichana, huku Adonis Djimali akipata nafasi ya pili. Katika kipengele cha usomaji wa Qur'an', Ammar Hoxha alipata nafasi ya pili na Yunus Bajaziti nafasi ya tatu; kwa upande wa wasichana, Riana Eyvazi alishika nafasi ya pili.

Mustafa Efendi Dalko, mwakilishi wa Msikiti Mkuu wa Kosovo, alikuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la kimataifa la majaji. Alisisitiza kuwa majaji walizingatia viwango vya juu vya umakini, uadilifu na usawa katika tathmini zao, akibainisha kuwa kiwango cha washiriki kilikuwa cha juu na ushindani ulikuwa mkali.

Sami Al-Awaji, mkuu wa jopo la majaji, pamoja na wajumbe wengine wa jopo hilo, waliusifu utendaji wa ujumbe wa Kosovo. Walisema ujumbe huo ulipata matokeo bora zaidi katika mashindano hayo, na kwamba mafanikio ya wawakilishi wake yanaonyesha kiwango cha juu kilichofikiwa na taasisi za elimu ya Qur'ani Tukufu nchini Kosovo.

3498511

captcha