IQNA

Jordan yatoa onyo kali kuhusu hatua haramu za Israel dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa

9:46 - August 07, 2026
Habari ID: 3482595
IQNA – Jordan imetoa onyo kali kwa washirika wake wa kimataifa kwamba utawala haramu wa Israel unaweza kuwa karibu kuchukua udhibiti kamili wa msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa AL Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Jordan imeonya kuwa hatua za hivi karibuni za utawala wa Israel katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa huko al-Quds zinaashiria kuwa unyakuzi wa eneo hilo unaweza kuwa “karibu kutokea,” hali inayozua hofu kuwa kubadilisha hali ya sasa (status quo) iliyodumu kwa muda mrefu kunaweza kuchochea mgogoro mkubwa wa kidini.

“Tunaonya kwamba kuchezea hali iliyopo… kunaweza kusababisha mgogoro wa kidini ambao utaenea nje ya Palestina na Jordan hadi ulimwengu mzima wa Kiislamu,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman Safadi, aliambia The Guardian. “Tunajaribu kuelezea hatari iliyopo. Tunalalamika kisheria. Tunajaribu kuongeza uelewa kuhusu hatari inayokuja kutokana na mwendelezo wa hatua hizo za Israel.”

Alisema matukio ya hivi karibuni katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa mara kwa mara wa mawaziri na wanaharakati wa kidini wa Israel, yanahatarisha kusababisha mgogoro mpana wa kidini kote kanda hiyo.

Onyo hilo linafuatia uvamizi wa Julai 23 katika eneo hilo uliofanywa na waziri wa usalama wa taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, pamoja na maelfu ya watu wenye itikadi kali ya Kiyahudi, walioingia chini ya ulinzi wa polisi, wakisali, kupeperusha bendera za Israel na kuimba wimbo wa utawala huo, jambo lililozua lawama kubwa kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Maafisa wa Jordan pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu ripoti za juhudi za kuunda kitengo maalum cha polisi kwa ajili ya lile wanaloliita “Temple Mount,” na wanaogopa changamoto zaidi dhidi ya ulezi wa Jordan wakati wa sikukuu kubwa za Kiyahudi baadaye mwaka huu.

Msikiti wa Al-Aqsa ni eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu na moja ya maeneo nyeti zaidi ya kidini katika mgogoro kati ya Israel na Palestina. Israel ilivamia Mashariki mwa al-Quds, ikiwemo Mji Mkongwe, wakati wa Vita vya Kiarabu na Israel vya mwaka 1967 na baadaye kulinyakua eneo hilo lililozaporwa, hatua ambayo haitambuliwi na jamii nyingi ya kimataifa.

Hata hivyo, Jordan imekuwa ikitumikia kama mlezi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo ya al-Quds kwa zaidi ya karne moja chini ya jukumu lililothibitishwa katika mkataba wake wa amani wa mwaka 1994 na Israel.

Safadi alisema mkutano wa dharura wa Jumatano utawakutanisha mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na Uturuki, Indonesia, Malaysia na Pakistan ili kujadili hali hiyo ambayo Jordan inaiona kuwa ya dharura.

Waziri huyo pia alielezea wasiwasi wake kuhusu jaribio la Israel la kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi uliopo chini ya uvamizi kuelekea Jordan, akionya kuwa hatua hiyo itavuka “mstari mwekundu” kwa nchi yake na kuhatarisha kuleta kuyumba zaidi katika kanda.

“Msimamo wetu ni kwamba huu ni mstari mwekundu ambao hatutauruhusu kuvukwa. Tumeweka wazi kwa kila mtu kwamba tutafanya kila liwezekanalo kuzuia jaribio lolote la Israel la kuhamisha Wapalestina kuelekea Jordan,” alisema.

3498544

Habari zinazohusiana
captcha