IQNA

Waislamu wakishikamana na Qur'ani, Umma wa Kiislamu utastawi

17:56 - May 31, 2014
Habari ID: 1412786
Iwapo Waislamu wa maeneo yote duniani wataweka kando migongano yao na kushikamana na Kamba ya Allah, yaani Qur'ani Tukufu, basi ulimwengu wa Kiislamu utashuhudia ustawi mkubwa na wa kasi katika nyanja zote.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa Shirika la Habari za Qur’an la Kimataifa IQNA, Abdul Basit Muhammad Abdi mwakilishi wa Uganda katika Mashindano ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanayoendelea Iran ameyasema hayo na kuongeza kuwa, Waislamu wanapaswa kukumbuka kuwa wote kwa pamoja wanaiamini Qur'ani Tukufu na hivyo inapasa kuwa msingi wa Umoja wa Kiislamu.
Aidha ameashiria juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kustawisha utamaduni wa Qur'ani na kusema mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ni ishara ya mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika harakati za  Qur'ani. Aidha Abdi amewapongeza wananchi wa Iran kwa kushiriki kwa wingi katika harakati za Qur'ani kama vile mashindano ya Qur'ani. Kuhusu majaji katika duru hii ya mashindano, Abdi amesema kuwepo wataalamu waandamizi wa Qur'ani kama vile Sheikh Ahmed Ahmed Noaina na Ahmed Baysuni pamoja na wataalamu wa ngazi za juu wa Qur'ani kutoka Iran katika jopo la majaji ni jambo ambalo limeyafanya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran kuwa kati ya bora zaidi duniani kwa mtazamo wa utaalamu na uamuzi usiopendelea upande wowote.
Qarii huyo wa Uganda pia ameashiria mapenzi na heshima yake kwa hayati kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini MA. Halikadhalika ameitaja Iran kuwa ardhi ya Uislamu na Qur'ani.
Mashindano ya 31 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu nchini Iran yalianza mjini Tehran Jumatatu katika mkesha ya tarehe 27 Rajab sawa na Mei 27 na yanatazamiwa kuendelea hadi Juni 2.
1412334

captcha