Jiri Dvorak amesema kuwa, Kamati ya Afya ya Fifa imefanya uchunguzi na utafiti wa kina kuhusiana na afya za wachezaji katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kufikia natija hii kwamba, iwapo wachezaji Waislamu watakula vyakula vinavyohitajika, hawatadhoofika kimwili katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Drovak ameongeza kuwa, kamati hiyo imefanya uchunguzi wa kutosha, hivyo hakuna ulazima wowote kwa wachezaji kuingiwa na wasiwasi kutokana na michuano hiyo kuingiliana na mfungo wa mwezi wa Ramadhani. Wakati huohuo, Michel D'Hooghe Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya FIFA amesema kuwa, hakutakuwa na tatizo lolote kwani utaratibu utakuwa kama ule uliofanyika wakati wa michuano ya Olimpiki iliyofanyika 2012 mjini London, Uingereza. Inatarajiwa kwamba, Waislamu wataanza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani kuanzia siku ya Jumamosi au Jumapili ijayo.