IQNA

Mkutano wa 38 wa Waislamu Amerika ya Kusini na Karibiani Wafanyika Brazil

15:25 - November 22, 2025
Habari ID: 3481553
IQNA – Mkutano wa 38 wa Kimataifa wa Waislamu wa Amerika ya Kusini na Karibiani unafanyika nchini Brazil, ukikusanya viongozi wa Kiislamu kujadili mada ya vijana Waislamu katika enzi ya akili mnemba (AI).

Jamii za Kiislamu kutoka Amerika ya Kusini na Karibiani zimekusanyika mjini São Bernardo do Campo, Brazil, kwa hafla ya ufunguzi wa mkutano huu. Tukio hili limeandaliwa na Centro de Divulgación del Islam para América Latina y el Caribe (CDIAL) kwa ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Kiislamu, Da‘wah na Mwongozo ya Saudi Arabia, na limeanza tarehe 21 Novemba.

Kikao kikuu kimefanyika katika ukumbi wa baraza la manispaa wa São Bernardo do Campo, na kuwaleta pamoja wawakilishi wa taasisi za Kiislamu na wageni kutoka Amerika ya Kusini na kwingineko.

Mada ya mwaka huu ni: “Vijana Waislamu katika Enzi ya Akili Mnemba: Fursa na Changamoto.” Washiriki wanajadili namna vijana Waislamu wanavyoweza kushughulikia mabadiliko ya kidijitali kwa kasi, changamoto za kimaadili katika teknolojia, na athari za akili mnemba katika maisha ya kila siku. Pia wanaangalia jinsi zana za kisasa za kiteknolojia zinavyoweza kuunganishwa na maadili ya Kiislamu, ili kukuza imani, maarifa na ufahamu kwa kizazi kijacho.

Waandaaji wamesisitiza kuwa mkutano huu wa kila mwaka ni jukwaa muhimu la mazungumzo, likiimarisha uhusiano kati ya mashirika ya Kiislamu katika ukanda huo. Wanasema unatoa nafasi ya kushughulikia changamoto za pamoja na kubuni mbinu bora za da‘wah katika dunia inayobadilika.

Kuanzia tarehe 22–23 Novemba, kila siku kutakuwa na vikao vya kielimu kuanzia saa 3:30 asubuhi kwa saa ya eneo, ambapo wasomi, watafiti na viongozi wa jamii watawasilisha mada kuhusu maadili, elimu, teknolojia na uongozi katika jamii ya Kiislamu.

CDIAL imezitaka jamii zote za Kiislamu nchini Brazil kushiriki kikamilifu katika matukio ya mkutano huu.

Mwaka jana, mkutano wa 37 ulifanyika mjini São Paulo kuanzia tarehe 29 Novemba hadi 1 Desemba, ukiwa na mada ya “Elimu ya Kidini Amerika ya Kusini na Karibiani na Nafasi Yake katika Kuhifadhi Utambulisho wa Kiislamu.” Zaidi ya wasomi, wahadhiri na viongozi wa jamii 120 kutoka nchi zaidi ya 30 walihudhuria, na kutoa mapendekezo ya kupanua elimu ya Kiislamu katika ukanda huo, kuanzisha shule zaidi za ndani, na kuimarisha mitaala ya Kiarabu na masomo ya Kiislamu.

3495477

Habari zinazohusiana
captcha