IQNA

Rais Hassan Rouhani

Matatizo ya Waislamu leo yametokana na kuiacha Qur'ani

7:46 - July 13, 2014
Habari ID: 1428807
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema matatizo wanayokumbana nayo Waislamu hivi sasa ni matokeo ya kutoyazingatia mafundisho ya Qur'ani Tukufu.

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumamosi usiku walipohutubu katika Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu mjini Tehran.  Akihutubu katika mahafali maalumu iliyofanyika kwa lengo la kuwaenzi wanaoihudumia Qur'ani, Rais Rouhani aliashiria sifa za kipekee za Qur'ani Tukufu. Alisema pamoja na kuwepo mitazamo tafauti katika kufahamu na kuifasiri Qur'ani Tukufu, lakini kwa bahati nzuri hakuna hitilafu kuhusu aya na yaliyomo katika Qur'ani Tukufu na hivyo kitabu hicho kitukufu ndio chanzo kikuu cha Umoja wa Kiislamu. Rais wa Iran Waislamu wanapojikurubisha na Qur'ani Tukufu huweza kufahamu maana ya aya za kitabu hicho kitukufu na hivyo kutekeleza maamurisho yake katika maisha.  Rais Rouhani amesema kusoma Qur'ani kwa sauti nzuri, kuiandika kwa maandishi mazuri na kuchapisha tarjuma na tafsiri zake ni hatua katika kukiarifisha kitabu cha Allah SWT kwa walimwengu. Rais wa Iran amesema njia pekee ya Waislamu kupata ukombozi ni kwa kufuata Qur'ani Tukufu, Mtume Muhammad SAW na Ahul Bayt Wake AS. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Rais Rouhani ameashiria hali ya mambo Palestina na jinai za kinyama za Wazayuni dhidi ya Wapalestina hasa huko Ghaza. Rais wa Iran amekosoa vikali kimaya cha jamii ya kimataifa kuhusu jinai hizo za Wazayuni. Katika hafla hiyo Rais Rouhani aliwatunuku zawadi watu 12 ambao wametoa huduma za kipekee kwa Qur'ani Tukufu hapa nchini Iran.
Akizungumza katika mahafali hiyo, Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu nchini Iran Dkt. Ali Jannati amewasilisha ripoti kuhusu Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu na kusema: "Serikali ya Iran inaamini kuwa tiba ya matatizo ya nchi za Kiislamu ni kushikamana na Qur'ani Tukufu, Mtume SAW na Ahul Bayt AS." Amesema iwapo Waislamu watachukua mkondo hao basi watweza kudumisha umoja wao. Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran amesema Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu mwaka huu yamejumuisha mashirika 252 ya uchapishaji, mashirika 55 ya program za kompyuta zinazohusiana na Qur'ani Tukufu na taasisi 66 zenye kutoa  suhula na huduma za kidijitali kuhusiana na Qur'ani Tukufu. Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu mjini Tehran yalianza tarehe 25 Shaaban na tanatazamiwa kumalizika tarehe 20 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
1428779

captcha