IQNA

Banki ya KCB Kenya kuanzisha rasmi mfumo wa Kiislamu

13:25 - July 31, 2014
Habari ID: 1434697
Banki ya KCB (Kenya Commercial Bank) nchini Kenya imetangaza kuwa itaanzisha rasmi mfumo kamili wa Kiislamu katika huduma za banki mwezi wa Agosti huku ikipanga kueneza huduma hiyo katika eneo lote la Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mkuu wa KCB , Joshua Oigara amesema banki hiyo sasa imepata kibali cha kuiwezesha kuanzisha mfumo wa Kiislamu katika huduma na bidhaa za banki katika matawi yake yote 182 nchini Kenya.
‘Mfumo wa Kiislamu katika huduma za banki ni moja ya ajenda zetu za kifedha ambapo tunaangazia namna ya kuleta bidhaa na huduma ambazo zitawafikia watu ambao hawatumii banki hadi sasa,’ alisema Oigara wakati akiwahutubia Waislamu ambao aliwaalika katika dhifa ya futari Jumatatu iliyopita mjini Nairobi.
Huduma hiyo ambayo itajulikana kama ‘KCB Sahal Banking’ inaenda sambamba na Shari’ah za Kiislamu na inalenga kuwahudhumia Waislamu ambao wanafungamana na imani ya dini yao tukufu inayokataza kutumia au kulipa riba.
KCB Tanzania pia inatua baadhi ya huduma za Kiislamu na inatazamiwa kuwa huduma mpya ya ‘KCB Sahal Banking’ itaimarisha bidhaa na huduma zilizopo za Kiislamu. KCB imesema bidhaa na huduma zake za kifedha za Kislamu zimeidhinishwa na Wanazuoni na Maulamaa wa Kiislamu. Jaafar Abdikadir ndie mkurugenzi wa  kitengo cha KCB cha mfumo wa Kiislamu katika huduma za banki. Amesema kuwa watategemea Maulamaa wa Kiislamu ili kuhakikisha kuwa huduma na bidhaa wanazotoa hazikikuki misingi ya Uislamu.  Amesisitiza kuwa mfumo wa Kiislamu katika huduma za banki utawalenga Waislamu na wasio kuwa Waislamu.
Katika miaka ya hivi karibuni huduma za kifedha za Kiislamu zimeimarika nchini Kenya na kote Afrika Mashariki kwa kufunguliwa benki kadhaa za Kiislamu na vile vile benki za kawaida zenye kutoa huduma maalumu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.

1434669

Kishikizo: kenya banki kcb kiislamu
captcha