IQNA

Maulamaa wa Kishia na Kisuni Uingereza wataka umoja wa Waislamu

7:37 - September 14, 2014
Habari ID: 1449625
Wanazuoni waandamizi wa Kishia na Kisunni nchini Uingereza wamefanya kikao cha pamoja na kujadili njia za kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu sambamba na kukabiliana na kampeni za kuibua fitina katika ulimwengu wa Kiislamu.

Katika kikao hicho cha Jumamosi, wanazuoni maarufu wa Kishia na Kisunni wameshiriki katika Kongamano la 18 la Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu mjini Birmingham ambapo wamejadili kwa kina suala la mazungumzo na kuheshimiana miongoni mwa madhehebu ya Kiislamu. Kongamano hilo la kila mwaka huandaliwa na Kituo cha Kiislamu cha England ambapo wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu hukutana kujadili matukio yanayowahusu Waislamu duniani. Mkuu wa kituo hichi Sheikh Mohammad Ali Shomali amesema ni jambo la kusikitisha kuona misimamo mikali ikipelekea mandugu Waislamu wasiweze kufanya kazi pamoja. Ametoa wito kwa Waislamu wote kushirikiana kama watu wa familia moja kwani wote ni ndugu. Naye Alammah Rabbani katibu mkuu wa Jammat Ahle Sunnat amesema makundi ya Kitakfiri katika nchi za Mashariki ya Kati ni 'magaidi halisi' ambao 'wanaliharibu jina la Uislamu kwa kuwaua watu wasio na hatia'. Kikao hicho cha Birmingham pia kilijadili njia za kukabiliana na propaganda ya vyombo vya habari vya Magharibi ambavyo vinapotosha ukweli na kudai kuwa ugaidi wa Matakfiri nchini Syria na Iraq ni vita vya Shia na Sunni. Washiriki katika kikao hicho wamesema matakfiri ni tishio kwa Waislamu wote.

1448474

captcha