Katika barua yake hiyo Ayatullah Rafsanjani amesema: katika kipindi hiki ambapo fitna mbalimbali zimeuandama Ulimwengu wa Kiislamu, kuzuia utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh An-Nimr kutawakatisha tamaa waleta mifarakano na kuimarisha umoja baina ya Shia na Sunni katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika sehemu nyengine ya ujumbe wake huo, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria nafasi ya kuwa na moyo wa uchukulivu na usamehevu katika Uislamu na taathira ya upendo katika kuziunganisha nyoyo na kueleza kwamba matarajio ya Waislamu kwa Mfalme wa Saudia ni kuchukua uamuzi wa tadbiri wa kuzuia kutekelezwa hukumu iliyotolewa dhidi ya alimu huyo wa Kishia. Sheikh An-Nimr, mujtahidi wa Kishia na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia alitiwa nguvuni kufuatia maandamano ya mwaka 2012 ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo. Tarehe 15 mwezi huu, mahakama ya jinai ya Saudia ilimhukumu adhabu ya kifo Sheikh Nimr Baqir An-Nimr kwa tuhuma za kufanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa taifa. Hadi sasa umeshatolewa wito na harakati na makundi mbalimbali ya Kishia katika kila pembe ya dunia kuitaka serikali ya Saudia izuie kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni huyo…/mh