IQNA

Rouhani: Kurejea katika Qur'ani, njia pekee ya kuokoka Waislamu

20:09 - January 01, 2015
Habari ID: 2665230
TEHRAN –IQNA–Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa njia pekee ya kuokoka Waislamu katika hali ya hivi sasa duniani ni kurejea katika mafundisho ya Kiislamu.

Rais Rouhani ameyasema hayo  leo alasiri mjiini Tehran alipohutubu katika ufunguzi wa Mashindano ya Tano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu. Katika hotuba yake, Rais Rouhani aliongeza kuwa Qur'ani Tukufu ndio chimbuko muhimu la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na miongoni mwa Waislamu. Ameendelea kusema kuwa nukta zingine zinazowaleta pamoja Waislamu ni Sala, Zaka, Hija, Jihad, kuamurisha mema na kukataza mabaya.
Rais wa Iran amesema kubakia nyuma Waislamu kimaendeleo kunatokana na kuiweka mbali Qur'ani Tukufu na kwamba, 'Qur'ani Tukufu ndio yenye kuwafungulia Waislamu njia ya kuokoka na kufikia ustawi, maendeleo, ustaarabu, umoja, udugu na kujiamini.' Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Qur'ani Tukufu imemfungulia mwanadamu njia ya kutafakari na kuongeza kuwa, 'Kitabu hiki kitukufu ni chanzo cha rehma, baraka na nuru kwa watu wa dunia.' Rais Rouhani amesema kuwa hakuna shaka kuwa Qur'ani Tukufu na Ahul Bayt AS  ndio sababu ya kuongoka Waislamu baada ya maisha ya Mtume Mtukufu wa Uislamu, Mohammad SAW.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa  Qur'ani Tukufu imetoa muongozo sahihi kwa mwanaadamu  na kuongeza kuwa , 'Iwapo kwa kutegemea muongozo wa Qur'ani Tukufu Waislamu watajiamini, kudumusha umoja na kurejea katika utambulisho wao wa Kiislamu, basi wanaweza kujenga mustakabali mwema katika nchi za Kiislamu.
Mashindano ya Tano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu yanaaza leo Alkhamisi katika ukumbi wa Mnara wa Milad  katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran. Mashindano hayo ya siku nne yana washiriki 66 kutoka nchi 47 ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu na watashindana kusoma (qiraa) na kuhifadhi Qur'ani Tukufu.../mh

2664196

captcha