Akihutubu leo katika ufunguzi wa Mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa Tehran, Rais Rouhani amesema hivi sasa kuna ardhi za Kiislamu zenye umuhimu wa kistratijia ambazo zinakaliwa kwa mabavu na madola ya kibeberu huku utajiri wa nchi hizo ukiporwa kutokana na migongano iliyoibuliwa. Rais Rouhani amesema kuna kundi la mamuluki wanaochafua taswira ya Uislamu kwa kufanya jinai nchini Iraq na katika mataifa mengine ya Kiislamu kwa kutumia jina la Uislamu.
Rais Rouhani ameongeza kuwa magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh (ISIL) wanachafua sura ya Uislamu kwa kuwaua kinyama watu wasio na hatia. Ameongeza kuwa, "Tunapaswa kuufahamisha ulimwengu kuwa Uislamu si dini ya vita na mabavu bali ni dini ya maelewano."
Rais wa Iran amesisitiza haja ya kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu huku akitoa wito kwa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo kuimarisha umoja. Ameongeza kuwa, wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa Waislamu kote duniani wanaungana na kuwa na mshikamano. Rais Rouhani amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itamtetea kila Mwislamu ambaye anasimama kupinga mabavu, ugaidi na ukaliaji mabavu.
Mamia ya wanazuoni wa madhehebu ya Shia na Sunni kutoka nchi 60 duniani wanashiriki katika kongamano hilo la siku tatu ambalo kauli mbiu yake ni, 'Umma Moja wa Kiislamu: Changamoto na Mikakati.../mh