IQNA

Mkutano wa Kimataifa wa ‘Ghaza, Nembo ya Muqawama’

13:56 - January 19, 2015
Habari ID: 2728172
Kongamano la Tano la Kimataifa la “Ghaza, Nembo ya Muqawama (mapambano)” lilifanyika hapa Tehran siku ya Jumapili kwa minajili ya kukumbuka na kuadhimisha siku ya ushindi mkubwa wa wanamapambano wa Palestina katika vita vya siku 22 vya Ghaza vilivyoanza mwishoni mwa mwaka 2008 na kuendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2009.

Katika vita hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel ulitekeleza hujuma ya kinyama dhidi ya eneo lililo chini ya mzingiro la Ukanda wa Ghaza.

Leo Tarehe 19 Januari inasadifiana na kumalizika vita hivyo vya siku 22 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Hivyo ni vita ambavyo vilimalizika kwa utawala wa Kizayuni kupata pigo na kushindwa kwa madhila kufuatia mapambano shupavu ya wapigania ukombozi wa Palestina. Katika takwimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tarehe 19 Januari inakumbukwa kama ‘Siku ya Ghaza’. Kongamano la Kimataifa la ‘Ghaza, Nembo ya Muqawama’ mwaka huu limejadili maudhui kuu zifuatazo; ‘Mapambano, Fursa na Changamoto’, ‘Tathimini Kuhusu Maelewano na Wazayuni’, ‘Tathmini kuhusu Makabiliano na Utawala wa Kizayuni Katika Eneo’, ‘Mapambano, Maelewano na Mikataba ya Kimataifa’ na ‘Quds, Mhimili wa Umoja wa Ulimwengi wa Kiislamu’.

Kati ya waliozungumza katika kongamano hilo ni pamoja na, Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, Nasser Abu Shariff mwakilishi wa Harakati ya Jihad Islami nchini Iran na Dkt. Zahra Mostafavi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kuunga Mkono Palestina. Aidha kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya mabalozi wa nchi za Kiislamu akiwemo Balozi wa Palestina nchini Iran.

Katika hotuba yake, Ali Larijani aliashiria namna Wapalestina wanavyopambana na utawala ghasibu wa Israel na kusema kwa yakini Wapalestina watapata ushindi katika mustakabali kwani wamepata nguvu kutokana na wimbi la mwamko wa Kiislamu katika eneo. Larijani amesema mapambano ya miongo kadhaa ya umma wa Kiislamu ni aina fulani ya mwamko ambao umevuka mipaka ya kijiografia. Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa kadhia ya Ghaza mbali na kuonyesha kudhulimuwa taifa la Palestina pia inaibua huzuni na kwa upande wa pili ni chanzo cha fakhari. Dkt. Larijani aidha ameashiria njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na kuelezea masikitiko yake kuhusu vitendo viovu vya Wazayuni katika msikiti huo ambao ni Qibla cha kwanza cha Waislamu. Spika wa Bunge la Iran pia amelaani vitendo vya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW na kusema vitendo kama hivyo vitaimarisha azma ya mapambano na muqawama miongoni mwa Waislamu.

Kwa upande wake, Bi. Zahra Mostafavi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kuunga Mkono Palestina amesema njia muafaka ya kuleta mabadiliko ya kimsingi katika kadhia ya Palestina ni eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kujiunga na mapamabano ya Wapalestina kama ilivyo Ukanda wa Ghaza. Amesema hatua hiyo itaweza kuimarisha mapambano dhidi ya Israel na kukomboa ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Dkt. Mostafavi ameongeza kuwa, kuunga mkono viongozi wa Palestina pendekezo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kujiunga na muqawama Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan  ni jambo linaloashiria kuigwa mfano wa Ghaza jambo ambalo hivi sasa ni takwa la umma. Kwa upande wake, Nasser Abu Sharif mwakilishi wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina hapa Iran ameonya kuhusu njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya Quds Tukufu na Msikiti wa Al Aqsa. Amesema kadhia ya Palestina haipaswi kuishia Ghaza tu kwani Ghaza ni nembo ya mapambano yote ya Wapalestina.../mh

2723831

captcha