Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo jana katika sherehe za kuwakumbuka mashahidi wa Quneitra na kuongeza kuwa, hivi sasa utawala wa Kizayuni unaishi katika hali ya wasiwasi mkubwa tangu ulipofanya shambulio lake dhidi ya wanamapambano wa Hizbullah huko Quneitra nchini Syria na kwamba woga huo unatokana kuwa Israel inafahamu fika kwamba muqawama umejiandaa kwa vita. Aliongeza kuwa, asubuhi ya siku ya Jumatano jeshi la adui (Israel) lilifahamu kuwa ni lazima Hizbullah ingetoa jibu kwa kuuliwa wanamapambano wake lakini hata hivyo askari hao wa Israel hawakuweza kuzuia shambulizi hilo, jambo ambalo linaonesha udhaifu mkubwa lilio nao jeshi la adui Mzayuni. Amesema kuwa, shambulizi la muqawama katika eneo la Shabaa, limeudhihirishia utawala wa Kizayuni kwamba, sasa unakabiliwa na nguvu kubwa ya wanamuqawama. Amesema kuwa, ubora wa shambulizi hilo la Shabaa, ni kwamba lilifanyika katika hali ambayo utawala wa Kizayuni ulikuwa umejiweka tayari kuzuia jibu la wanamuqawama lakini bila mafanikio, na kuongeza: "Walituua mchana Quneitra, na sisi tukawaua mchana (Shabaa). Walitushambulia kwenye magari mawili, na sisi tukawashambulia kwenye magari mawili na kuua wengi kati yao." Amesema, Israel imeficha habari kuhusu idadi ya askari wake waliouawa huko Shabaa, katika hali ambayo wanamapambano waliweka wazi idadi ya mashahidi wake waliouawa katika eneo la Quneitra. Ameongeza kwamba wanamapambano wa Hizbullah waliwaendea Wazayuni bila kujificha tena uso kwa uso, katika hali ambayo Israel ilifanya shambulizi lake kwa uficho na kwa siri, hali inayoonyesha khofu ya Wazayuni kwa wanamapambano wa Harakati hiyo ya Hizbullah ya nchini Lebanon.../mh