Barua ya Sinwar siku ya Ijumaa imeandikwa kujibu ujumbe wa rambirambi wa Sayyid Hassan Nasrallah kufuatia mauaji ya kiongozi wa zamani wa Hamas Ismail Haniyah mjini Tehran.
Katika barua hiyo, Sinwar akiashiria kufa shahidi Ismail Haniyah na mlinzi wake katika shambulizi hilo la kigaidi lililotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel amesema: "Sisi katika Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina tumepokea kwa shukrani na fahari ujumbe wako mzuri wa kuwaomboleza mashahidi wetu wawili na masahibu wako katika jihadi na muqawama."
Haniyah aliuawa shahidi katika makazi yake katika nyumba ya wageni kaskazini mwa Tehran baada ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.
Sinwar alimsifu Haniyah kama "nembo ya taifa la Palestina", akisema damu yake na damu ya Wapalestina wengine itaongeza nguvu na uwezo wao "katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Kinazi".
Aidha kiongozi huyo wa Hamas ametoa mfano wa umoja wa watu wa Palestina katika kuchagua jihadi na muqawama, na umoja wa taifa katika kukabiliana na mradi wa Kizayuni na kusema Wapalestina watalinda matakatifu yao ambayo ni mji wa al-Quds na Msikiti wa al-Aqsa.
3489880