IQNA

El Baradei ajibu hujuma za kigaidi Sinai Misri kwa aya ya Qur’ani

17:03 - January 31, 2015
Habari ID: 2790529
Makamu wa zamani wa rais wa Misri Mohammad El Baradei Ijumaa ametuma aya ya Qur’ani kupitia mtandao wa kijamii wa twitter kujibu hujuma za kigaidi zilizotekelezwa na wanamgambo katika eneo la Sinai nchini Misri ambapo watu 30 waliuawa.

El Baradei katika akaunti yake ya twitter amenukulu sehemu ya aya ya 32 ya Surat Al Maida isemayo kuwa:…
«مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَیْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِی الأَرْضِ فَکَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِیعًا»
….aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote….
Al Baradei ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Nyuklia IAEA alikuwa makamu wa rais wa Misri anayeshughulikia masuala ya kimataifa kuanzia Julai 14 2013 hadi  Agosti 14 2013 wakati alipojiuzulu baada ya vikosi vya usalama kuwashambulia wafuasi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin mjini Cairo ambapo mamia ya watu waliuawa.
Ikumbukwe kuwa Alkhamisi wiki iliyopita watu wasiopungua 30 waliuawa katika hujuma ya kigaidi katika Peninsula ya Sinai huko kaskazini mwa Misri. Baadhi ya duru zinasema watu 45 waliuawa katika hujuma hiyo ambayo kundi moja lenye mfungamano na magaidi wa Daesh (ISIS)  limetangaza kuitekeleza.../mh

2789329

captcha