Ayatullahil-Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo alipokutana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, ambapo akiashiria mazungumzo ya nyuklia alisema: timu inayoliwakilisha taifa la Iran katika mazungumzo hayo, kiinsafu ni nzuri, aminifu, yenye kukubalika, yenye uchungu na maslahi ya taifa na inafanya juhudi kubwa katika suala hilo. Ameongeza kuwa, hata hivyo na licha ya juhudi hizo upande wa pili ambao ni hodari kwa kufanya hila na ujanja, unaifanyia usaliti timu hiyo ya Iran. Akiashiria makosa yanayofanywa na wengi kudhani kwamba watu wenye nguvu kawaida huwa hawahitaji kufanya hila, Ayatullah Khamenei amesema: baadhi wanadhani kwamba, licha ya uwezo mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi, ilionao Marekani, haihitaji kufanya ujanja na hila, lakini ni kinyume na dhana hiyo, kwani Washington inahitaji sana mambo hayo na hivyo ndivyo inavyofanya hivi sasa; na ukweli huu unatutia wasi wasi mno. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria barua ya hivi karibuni ya maseneta wa Marekani ambayo amesema ina nukta kadhaa zinazoakisi kuporomoka kwa maadili ya kisiasa katika utawala wa nchi hiyo na kufafanua kwamba, nchi zote za dunia zinafuata mikataba iliyoainishwa kimataifa hivyo hata baada ya kujiri mabadiliko ya kiserikali, nchi hizo huendelea kufungamana na kuheshimu mikataba ya hapo awali. Hata hivyo kwa bahati mbaya maseneta wa Marekani wametangaza rasmi kwamba, ikiwa serikali ya sasa itamaliza muda wake, wataichukulia mikataba hiyo kama haikuwepo. Akizungumzia suala la ugaidi, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Marekani na waitifaki wake katika eneo ndio walioanzisha kundi habithi na ovu zaidi la kigaidi yaani Daesh na mengineyo na wanaendelea kuyaunga mkono makundi hayo kisha wanalihusisha na vitendo hivyo taifa la Iran na mfumo wake wa Kiislamu.../mh